Ressources numériques en sciences humaines et sociales OpenEdition Nos plateformes OpenEdition Books OpenEdition Journals Hypothèses Calenda Bibliothèques OpenEdition Freemium Suivez-nous

Sehemu ya #1. Hotuba ya Tundu Lissu ya tarehe 3 Aprili 2025, “Tutakinukisha: ‘Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi’”

Nicodemus MINDE & Marie-Aude FOUÉRÉ, “Sehemu ya #1. Hotuba ya Tundu Lissu ya tarehe 3 Aprili 2025, “Tutakinukisha: ‘Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi’” Mambo! no. 106, 2026

Tindu Lissu katika Mahakama Kuu, Dar es Salaam, 20 Februari 2026; kwa hisani ya akaunti ya X ya Chadema

Tarehe 21 Januari 2025, Tundu Lissu alimshinda Freeman Mbowe katika uchaguzi wa ndani wa CHADEMA (Chama Cha Demokrasia na Maendeleo) na akawa mwenyekiti mpya wa chama. Maswali mawili muhimu yaliibuka mara moja: Je, chama kingeweza kustahimili mabadiliko haya kutoka kwa Mbowe, mwanasiasa mzoefu aliyekuwa kiongozi wa chama kwa zaidi ya miaka ishirini na mtetezi wa hali ya kisiasa iliyokuwepo (status quo), hadi kwa Lissu, anayejulikana kama kiongozi mwenye msimamo mkali (Minde, 2024)? Na chama tawala cha muda mrefu CCM (Chama Cha Mapinduzi), ndani ya mfumo wa chama kimoja wa kiimla (Makulilo, 2008; Paget, 2019), kingejibu vipi?

Chini ya Mbowe, CHADEMA kiligeuka na kuwa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania kwa kujenga uungwaji mkono imara wa kutoka ngazi ya chini kitaifa. Hii ilikuwa mafanikio makubwa chini ya serikali iliyojikita kwenye mfumo wa chama kimoja. Kwa ushindi wa Lissu na viongozi wapya, miongoni mwao John Heche (Makamu Mwenyekiti), John Mnyika (Katibu Mkuu) na Godbless Lema ambaye ameonyesha uthabiti, chama kilikuwa kinaelekea kupita katika wimbi la siasa za upinzani nchini Tanzania kwa njia mpya. Hii ilikuwa changamoto kwani CHADEMA ilikuwa imechukua msimamo wa ‘Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi’ wakati wa mkutano mkuu wa chama Desemba 2024. Ilimaanisha kuwa hakingeshiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 bila mageuzi muhimu ya uchaguzi na kisiasa kufanyika kwanza (Minde, 2025). Wakati kundi moja, lililoegemea upande wa Mbowe, liliona hili kama mbinu ya kushinikiza ili kupata mageuzi, kundi lingine, lililoegemea upande wa Lissu, lilikuwa tayari kwa kususia uchaguzi.

Lissu alitoa tafsiri ya kauli mbiu ya ‘Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi’ alipokuwa akiwahutubia wagombea wa chama hicho tarehe 3 Aprili. Hotuba yake, ambayo tumeipa kichwa “Tutakinukisha: ‘Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi’”, ilikuwa tamko la kimpango, uzungumzaji wa balagha (rhetorical) na hatua ya makusudi ya kuipa CHADEMA mwamko mpya na kugeuza mapambano ya kisiasa ya Tanzania kama suala la ukombozi badala ya ushindani (wa kiuchaguzi).

Siku chache baadaye, tarehe 9 Aprili 2025, Lissu alikamatwa mjini Mbinga, mji ulioko kusini mwa Tanzania, alipokuwa akihutubia wafuasi wa CHADEMA. Alipelekwa usiku kucha hadi Dar es Salaam na, tarehe 10 Aprili 2025, alishtakiwa rasmi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu kwa makosa mawili: uhaini na uchapishaji wa taarifa za uongo. Jalada la mashtaka la upande wa mashtaka lilielekeza kwenye hotuba aliyotolewa na Lissu tarehe 3 Aprili 2025, ambayo serikali (upande wa mashtaka) ilidai ilikuwa ikitoa wito wa kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Ingawa tunatambua tafsiri ya kisheria ya serikali kuhusu hotuba ya Lissu, lengo letu ni kufanya usomaji wa kina na ukaribu pamoja na kutaka kuelewa matamshi yake, maana na umuhimu wake. Hotuba ya Lissu ni tukio la kisiasa lililotokea katika muktadha maalum linalojumuisha simulizi za kihistoria, kujitolea binafsi, maadili ya kisiasa, na utata wa kimkakati. Inaweza kuchukuliwa kwa wakati mmoja kama tendo la maonyesho (performative) na kielelezo cha kitu (materiality) (Barber, 2007) ili kutoa dhana ya balagha (rhetoric). Uhusiano kati ya maandishi na utu (personhood) pia ni kipengele muhimu cha hotuba: wasifu wa Lissu—kama vile mateso aliyopitia, uwezekano wa kukamatwa, na kuachana na malengo ya uchaguzi—umefumwa katika muundo wa kihotuba, ukitengeneza mada ya kisiasa ndani ya maandishi yenyewe. Hivyo basi, uhalali huzalishwa na muafaka kati ya hotuba, historia binafsi, na jinsi hadhira inavyotarajiwa kupokea.

“Tutakinukisha: ‘Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi’”

Hotuba hii ya Tundu Lissu inapatikana kwenye YouTube, 11 Mei 2025: https://www.youtube.com/watch?v=KkIZj15NurU

“Wamesema kitu kimoja, kitu sahii hapa, wanasema hivi…

Msimamo huu [Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi], unaashiria uasi…ni kweli, ni kweli

Akisema “Wamesema”, Lissu anamaanisha wanasiasa na wafuasi wa CCM. Samia Suluhu Hassan alipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2021, kufuatia kifo cha John Magufuli, alianzisha mageuzi kadhaa na kugeuza sera nyingi za mtangulizi wake. Hata hivyo, mageuzi haya yalionekana kuwa ya juu juu na hayakuwa yamejikita katika mageuzi ya kitaasisi au kikatiba. Mara kwa mara, nchi ilipokaribia uchaguzi wa Oktoba 2025, mageuzi mengi kati ya haya yalirejeshwa na ukandamizaji wa serikali uliongezeka.

Kwasababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi,

Hio ndio namna ya kupata mabadiliko, [Makofi]

Ndio namna ya kupata…

CHADEMA inapinga utawala wa kiimla wa uchaguzi Tanzania (electoral authoritarianism)—mfumo ambapo uchaguzi unafanyika lakini unaendeshwa chini ya mazingira ya kimabavu (angalia Schedler 2006; Levitsky & Way, 2010; Riedl, 2014). Licha ya kufanya uchaguzi wa vyama vingi mara kwa mara, utawala wa kiimla wenye ushindani ndio utaratibu nchini Tanzania (Morse, 2014), unaojulikana kwa ushiriki mdogo wa upinzani, vizuizi kwa vyombo vya habari, na kupunguzwa kwa haki za kiraia na kisiasa. CHADEMA, kwa mfano, inataja uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019, ambao chama tawala CCM ulishinda kwa kishindo na, uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ambapo Magufuli aliyekuwa madarakani alishinda kwa asilimia 85, na uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024. Katika chaguzi zote hizi, upinzani ama ulinyamazishwa kimfumo kwa kuwaondolewa wagombea, kukamatwa kwa viongozi wakuu wa upinzani, au unyanyasaji wa polisi. Chini ya hali kama hizi, chaguzi hazionekani kama michakato ya kidemokrasia iliyo wazi, bali kama michakato inayotumiwa kuhalalisha mfumo usio na haki.

Mandela had to go through 27 years, by treason ili kupata mabadiliko Afrika Kusini.

Marejeleo ya Lissu kwa Nelson Mandela yanaimarisha hoja yake kwamba yuko tayari kwenda gerezani katika mapambano ya kuikomboa Tanzania kutoka kwa utawala wa kiimla. Hotuba yake inaweza kulinganishwa na hotuba ya Mandela katika Kesi ya Rivonia tarehe 20 Aprili 1964, ambapo kiongozi huyo wa Afrika Kusini alitangaza utayari wake kufa kwa ajili ya mapambano ya watu wa Afrika Kusini (Mandela, 1964). Baadaye katika hotuba yake (tazama hapa chini), Lissu anataja viongozi wengine wakuu wa Afrika wakati wa mapambano ya ukombozi waliofungwa gerezani wakati wa mapambano dhidi ya ukoloni, akiwataja Kenneth Kaunda, Robert Mugabe, Sam Nujoma na Jomo Kenyatta.

Kwahio, kwahio, tunaenda kukinukisha. [Makofi]

Wakati wa kikao cha Mahakama Kuu cha tarehe 8 Oktoba 2025, Lissu, ambaye hadi wakati huo alikuwa ameanza kujitetea mwenyewe, anamhoji shahidi mmoja wa upande wa serikali kuhusu maana ya kukinukisha. Lissu analinyambua neno la Kiswahili kunuka, ambalo linaashiria harufu mbaya (nuka), na kunukia, ambalo linamaanisha kunukia vizuri. Hapa, Lissu siyo tu anabashiri kitendo; anatekeleza ahadi, akiweka nafasi yake na hadhira yake ndani ya hali mpya ya kisiasa iliyoundwa.

Waliotayari tutakwenda nao, tunakwenda na walio tayari.

Hakuna mtu atakayewekewa bunduki hapa, walio tayari tutaenda nao.

Wanaofikiria kwamba CCM watakua walokole, wamebadilika na nini…, tunawakatika kila la heri.

Sisi sio watu wenye roho mbaya…

Lakini kama unataka kuwa mbunge kusema ukweli…

Twende tukapiganie mabadiliko

Tukapiganie mabadiliko ndugu zangu…

Miito ya mara kwa mara ya ujumuishi ya Lissu, ‘ndugu zangu’, na amri za moja kwa moja kwa nafsi ya pili, kama ‘msiogope’, huimarisha umoja wa kimaadili na kisiasa unaofafanuliwa zaidi na utayari wa pamoja wa kuchukua tahadhari ya kisiasa ya muda mrefu ya kutokushiriki katika uchaguzi ikiwa hakuna mageuzi muhimu. Hotuba zinapaswa kuonekana kama vitendo vya kijamii vinavyounda hadhira (publics), sura za mzungumzaji (authorial personas), na nyanja za tafsiri (interpretive fields), badala ya kuwa njia za kupitisha maana bila kuchangia (Bauman, 1985; Barber, 2007). Hotuba ya Lissu hailengi tu hadhira iliyopo: inaipa hadhira uhai.

Kitu gani kitachoharibika?

Kitu gani ambacho…

Nchi itapotea? Sana sana…tutavuruga huu uchaguzi…

Kama unafikiria kuwa mbunge Oktoba au Novemba, sahau… hio ni kweli… hio ni kweli

Na mimi nilikua nafikiria urais, na mimi nilikua nafikiria urais, ni mtia nia… nimesahau.

Kama ulikua unafikiria udiwani Novemba sahau.

Kwasababu tunakwenda kukinukisha vibaya sana. Sawa sawa? [Peoples, Peoples Chants]

Tukikinukisha vile, tukikinukisha vile

Tutaumia, ni kweli, ni kweli

Lakini, mimi nina imani tutashinda,

Unajua kwanini, unajua kwanini?

Tukikinukisha seriously, watafanya nini?

Watatua? Wanaweza?

Kwahio, mimi nimekinukisha, nakamatwa, nakamatwa.

Napelekwa wapi?

Naenda kushtakia kwa uhaini, kwa kuamsha maasi…

Actually, actually…hakuna…

Katika siasa za ukombozi, sizungumzii siasa za udalali, kwenye siasa za ukombozi. Siasa za udalali sio za ukombozi [Wasikilizaji wanaitika kwa kusema, ‘Peoples, Peoples, Power’– – kaulimbiu ya CHADEMA]

Kwenye siasa za ukombozi, kwenye siasa za ukombozi, kukamatwa na kushtakiwa mahakamani ni kuvikwa taji la dhahabu…okay…

Kwa kutaja ‘siasa za ukombozi’, Lissu anaipa CHADEMA nafasi si tu kama chama kinachoshindana ndani ya mfumo, bali kama chama cha kiharakati kinachopinga mfumo wenyewe. Matumizi ya neno ‘uasi’ na Lissu katika hotuba yake yote ni ya makusudi. Chini ya sheria za Tanzania, ‘uchochezi’ na ‘uasi’ ni mashtaka ambayo kihistoria yamekuwa yakitumika dhidi ya wapinzani. Lissu kwa mbinu anafuta nguvu ya unyanyapaa ya neno hili na kulibadilisha kuwa swali la kimaadili.

Ngoja nieleze hio…

Julius Nyerere [Ananyamaza kidogo]. Mara nyingi hatufahamu historia yetu…

Nani alikua Mtanganyika wa kwanza kupatikana na hatia ya kosa linaloitwa uchochezi?… [Wasikilizaji wanajibu] Nyerere

Kihistoria, CCM imekuwa ikitumia kumbukizi ya pamoja ya Julius Nyerere na urithi wake kuzalisha na kuendeleza dhana ya kuhodhi ama kuonyesha ubabe wa tafsiri ya maadili ya kisiasa (Fouéré, 2015; Minde, 2021). Upinzani unaweza kutumia mbinu ile ile kuvunja marejeleo ya dhana hii ya CCM na kuipa taswira mbadala ya Nyerere kwa mbinu tofauti (Kwayu, 2015).

Julius Nyerere, hio kesi ya Julius Nyerere ya mwaka 1958, yeye na mhariri wa TANU anaitwa Robert Makange wa gazeti la TANU na mhariri wa gazeti la Mwafrika anaitwa Rashid Kheri Baghdelee alikuja kuwa mbunge… Hio ilikua kesi iliyompaisha Nyerere beyond measure.

Kesi ya Julus Nyerere, alipatikana na hatia ya uchochezi. Kaambiwa afungwe miezi sita, aende jela miezi sita ama alipe shilingi 300…300 mwaka 1958 hazikua chache.

Lissu anataja kesi ya uchochezi ya Nyerere kabla ya uhuru, ambayo ilithibitisha urithi wa Nyerere katika ukombozi. Mnamo 1958, Nyerere, akiwa kiongozi wa Tanganyika African National Union (TANU), alishtakiwa kwa kosa la kashfa ya jinai au kashfa ya uchochezi na utawala wa kikoloni wa Uingereza. Kesi hiyo mara nyingi hujulikana kama kesi ya uchochezi nchini Tanzania. Wahariri wawili wa gazeti la Mwafrika, Kheri Rashid Baghdellah na Robert Makange, pia walishtakiwa kwa uchochezi na utawala wa kikoloni. Katika hati rasmi ya mashtaka, Nyerere alishtakiwa kwa kumtusi (kumkashifu) Kamishna wa Wilaya wa kikoloni Weeks wa Musoma katika mchango wake kwenye gazeti la TANU, pili, kumshutumu DC Scott wa Songea, na tatu, kushtakiwa kwa pamoja kwa kuwakashifu maafisa hao wawili (Ngh’waya, 1990). Kwa kusisitiza kwamba Nyerere alihukumiwa kwa uchochezi, Lissu anampa Nyerere taswira mbadala ya kiongozi ambaye aliwapinga na ‘kuwakashifu’ wasimamizi wa kikoloni na baadaye akawa kiongozi wa kwanza baada ya uhuru.

Na ukifikiria nani mwingine anayetuzunguka wa nchi zetu ambaye hakuenda gerezani…

Kaunda [Kenneth] alienda gerezani.

Mugabe [Robert] alienda gerezani.

Nujoma [Sam] alienda gerezani.

Kenyatta [Jomo] alienda gerezani… miaka 9.

Hotuba kama kitendo cha maonyesho (performative speech) inapata nguvu sio tu kwa uasilia wake, bali pia kwa kunukuu mambo yaliyo na uhalali. Lissu kuwanukuu mara kwa mara akina Mandela, Nyerere, na viongozi wengine wa ukombozi inatumika kama msururu wa nukuu, ukiimarisha maneno yake katika sarufi ya upinzani iliyokubaliwa kihistoria. Nguvu ya hotuba hiyo haitoki kwa mamlaka ya kisheria bali inatokana na uhusiano wake na historia ya pamoja ya mapambano ya ukombozi. Kwa maana hii, hotuba haitetei tu uasi; inaonyesha uasi kama kitendo cha kimaonyesho pamoja na dhana nyingine za kijamii, kama vile rangi, utaifa, na utambulisho wa kitaifa, kama miundo inayotambulika ya kisiasa.

Alipotoka gerezani, straight Lancaster House Kwenda kujadili uhuru.

Nyie mnasema hivi, ni uhaini, uasi, kwa hio tutafungwa…sion…ndio uasi? That is the way to freedom.

Lissu, ambaye amepitia ukandamizaji na mateso makali wa serikali hapo awali, anaelezea kifungo cha jela si kitendo cha kiukandamizaji bali ni kama tohara (rite of passage). Mnamo 2017, alinusurika jaribio la mauaji alipokuwa Mbunge. Anahusisha jaribio hilo la mauaji na juhudi zake za kufichua ufisadi serikalini na kutetea demokrasia na haki za binadamu. Ingawa hakumtaja waziwazi mtangulizi wake, Freeman Mbowe, ambaye pia alikamatwa na kushtakiwa kwa ugaidi, Lissu anaonyesha mwelekeo wa CHADEMA kuwa unaunga mkono juhudi za ukombozi. Ni kwa kupinga utawala wa kiimla uliopo ndipo unaweza kuleta mifumo mipya ya utawala bora.

Tutachelewa kidogo…kama hamu ni ubunge, tutachelewa kidogo. Lakini tutapata mageuzi yatakayo tupeleka wengi zaidi bungeni.

Watu wanataka twende tukapate asilimia 5 (ya kura) na wabunge labda 7 halafu tuanze kupigana vikumbo juu ya nani aende kwenye viti maalumu.

Nataka tupate kura nyingi zaidi, na tuna uwezo wa kupata kura nyingi zaidi, ili wote mnaotaka viti maalum mpate nafasi ya kua viti maalum.

Mtapata viti maalum kukiwa na mabadiliko, sio hii habari ya nini hii…

Na tutakua na wabunge wa majimbo wengi zaidi.

Na tutakua na rais, actually…

Kwahio, kwahio…ni njia ngumu, ni kweli…

Hakuna chama kimewahi kuzungumza lugha hii… [hakuna] katika nchi hii.

Ni sisi tunazungumza. Kwahio.. 

Kwahio wahemishimiwa, tujiandae, tutashinda.

Msiogope. Msiongope. Msigope.

Kwahio ndugu zangu, ya kwangu ni hayo.

Nimetoka kwenye ziara ya kanda ya Nyasa, na kesho tunaenda kusini. Mheshimiwa Mayala, kesho tuko kwako. Huko kanda ya Nyasa tulikotoka…Nimemuona Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa… Wako hapa watu wa Nyasa. Watu wa Nyasa embu simameni. Simameni wote. Hawa petitioners, wanasema hivi…

Aden Mayala alikuwa mwenyekiti wa CHADEMA wa kanda ya Kusini kabla hajahamia CCM muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu ya mwezi wa Oktoba 2025. Nyasa, kanda ya Kusini mwa Tanzania ambayo CHADEMA unautaja kama maabara ya kisiasa, hutumika kama kielelezo: mapambano yanaonyeshwa sio kama makabiliano ya wasomi tu bali pia kama hisia za wananchi wa kawaida. Hii inaakisi kauli za kimapinduzi zinazodai kugundua hasira ya umma badala ya kuziibua.

Hichi chama nilichikiona Nyasa kitakufa tusipoenda kwenye uchaguzi. Hawa ni watu ambao wamesahau kufanya siasa za wananchi wetu.

Lissu anakataa madai kwamba CHADEMA “itakufa” kama haitoshiriki uchaguzi, akisisitiza kwamba uhalali wa kisiasa unapaswa kutegemea siasa zinazolenga watu—ambayo ndiyo itikadi kuu ya chama (‘Nguvu ya Umma’) badala ya mitandao ya watu wa daraja la juu (elites). Analinganisha mkazo wa ustawi wa watu na uchumi wa kisiasa wa kieliti unaendana na unyakuzi wa rasilimali, miradi ya uchimbaji (kama vile uchimbaji madini), utoaji wa nafasi za kazi kwa wanufaika wa ufisadi. Katika mtazamo huu wa upopulisti, kushiriki katika uchaguzi bila kutekeleza mageuzi kunaonekana kama kuunga mkono utawala wa unyonyaji badala ya kukuza maslahi ya pamoja katika maendeleo.

Wananchi wa Nyasa ambao mimi nimekua nao kwa siku nane, wako militant hujawahi kuona.

Kama hao ndio Watanzania, wanachama wetu, ndio niliowaona Nyasa, nafurahi wako hivo kila mahali, basi tukapambane, tutapata mabadiliko. Tukapambane, tutapata mbadiliko.

Watu wetu wanahitaji kuandaliwa, wanahitaji kuongozwa na viongozi jasiri.

Tusiende na hii [dhana] ya kugusa unarudi, unagusa unarudi.

Hii sio namna ya kwenda. Sawa Sawa?

Kwahi ndugu zangu, ya kwangu ni hayo.

Niwashukuru sana watu wa Nyasa.”    

Mfululizo huu wa makala ya Mambo! unajikita katika kuelezea mwaka wa uchaguzi wa 2025 nchini Tanzania. Unatoa maelezo ya kipekee wa usomaji wa kina na ukaribu wa vielelezo vya matukio ya kisiasa ya mwaka huu wa uchaguzi, uliokua na matukio mengi na uliotawaliwa na muendelezo wa ukandamizaji wa serikali. Katika kila sehemu cha mfululizo huu, tukio lililochaguliwa linazalishwa tena katika asili yake na kutafsiriwa panapohitajika, likiwekwa katika muktadha kwa uangalifu na kufafanuliwa au kupewa maelezo ya karibu kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa kuelewa kwa kina sehemu lilipotokea pamoja na maana na umuhimu wake. Matukio haya ni vyanzo ama nyaraka ya maana kwa ajili ya kuchambua muendelezo wa utawala wa kimabavu na ukandamizaji wa wazi uliofanywa na serikali ya Tanzania katika kipindi hiki cha uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2025.

Marejeo

Barber, K. (2007). The anthropology of texts, persons and publics. Cambridge University Press. https://doi.org/10.1017/cbo9780511619656

Bauman, R. (1975). Verbal art as performance. American Anthropologist, 77(2), 290–311. https://doi.org/10.1525/aa.1975.77.2.02a00030

Fouéré, M.-A. (2015). “Julius Nyerere”: The man, the word, and the order of discourse. In M.-A. Fouéré (Ed.), Remembering Nyerere in Tanzania: History, Memory, Legacy (pp. 3–32). Mkuki wa Nyota/Africae. http://books.openedition.org/africae/703

Kwayu, A. C. (2016). Different “uses of Nyerere” in the Constitutional Review debates: a touchstone for legitimacy in Tanzania. In M.-A. Fouéré (Ed.), Remembering Nyerere in Tanzania: History, Memory, Legacy (pp. 128–140). Mkuki na Nyota/Africae. https://books.openedition.org/africae/758

Levitsky, S., & Way, L. A. (2012). Competitive authoritarianism: Hybrid regimes after the Cold War. https://doi.org/10.1017/cbo9780511781353

Makulilo, A. (2008). Tanzania: a de facto one party state? VDM Verlag.

Mandela, N. (1964, April 20). “I am prepared to die” [Comment on “Statement by Nelson Mandela from the Dock at the Opening of the Defence Case in the Rivonia Trial, Pretoria Supreme Court – Pretoria”]. http://www.mandela.gov.za/mandela_speeches/before/640420_trial.htm

Minde, N. (2021). The endurance of one-party dominance: the Chama Cha Mapinduzi (CCM) party and the challenge of democratizing the Tanganyika-Zanzibar Union. [PhD Dissertation]. United States International University-Africa.

Minde, N. (2024, October 18). Who is Tundu Lissu? Tanzania’s opposition leader is fighting for change in the face of fresh attacks on political freedoms. The Conversation. https://doi.org/10.64628/aaj.h3yq949hs

Minde, N. (2025). Stifling democracy in Tanzania: Scenarios for the 2025 elections. In ISS Africa (Policy Brief No. 206). https://issafrica.org/research/policy-briefs/stifling-democracy-in-tanzania-scenarios-for-the-2025-elections

Morse, Y. L. (2013). Party matters: the institutional origins of competitive hegemony in Tanzania. Democratization, 21(4), 655–677. https://doi.org/10.1080/13510347.2013.764285

Ngh’waya, S. (1990). Kesi ya Julius Kambarage Nyerere 1958. Tanzania Publishing House.

Paget, D. (2018). The authoritarian origins of well-organized opposition parties: The rise of Chadema in Tanzania. African Affairs, 118(473), 692–711. https://doi.org/10.1093/afraf/ady061

Riedl, R. B. (2014). Authoritarian origins of democratic party systems in Africa. Cambridge University Press.

Schedler, A. (2006). Electoral authoritarianism: The Dynamics of unfree competition. L. Rienner Publishers.


OpenEdition vous propose de citer ce billet de la manière suivante :
Nicodemus Minde, Marie-Aude Fouéré (2 mars 2026). Sehemu ya #1. Hotuba ya Tundu Lissu ya tarehe 3 Aprili 2025, “Tutakinukisha: ‘Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi’”. Mambo ! Consulté le 10 mai 2026 à l’adresse https://doi.org/10.58079/15siv


Vous aimerez aussi...

Laisser un commentaire

Votre adresse e-mail ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.