Ressources numériques en sciences humaines et sociales OpenEdition Nos plateformes OpenEdition Books OpenEdition Journals Hypothèses Calenda Bibliothèques OpenEdition Freemium Suivez-nous

Sehemu ya #2 Kuchora fedheha ya kimaadili ya Samia Suluhu Hassan: Katuni ya kisiasa ya Gado ya tarehe 1 Novemba 2025

Nicodemus MINDE, Marie-Aude FOUÉRÉ “Kipindi cha 2 # Kuchora fedheha ya kimaadili ya Samia Suluhu Hassan: Katuni ya kisiasa ya Gado ya tarehe 1 Novemba 2025Mambo! no. 107, 2026

Mnamo tarehe 1 Novemba 2025, katuni ya mchoraji Gado iligusa hisia za wengi. Ilimuonyesha rais mteule wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akiapishwa mbele ya Jaji Mkuu, mmoja wa mikono yake ukishikilia Qur’ani, na mwingine ukiwa juu ya Katiba, akiwa amesimama juu ya lundo la maiti zenye damu ambazo zulia lililozifunika halifanikiwi kuzificha. Mikono ya rais mteule, nguo zake, na hata Qur’ani yenyewe zimechafuka kwa damu. Wanaume wenye silaha wenye sura kali, nyuso zilizofunikwa na skafu na kofia za bereti zilizokuwa na alama ya fuvu la kichwa wanamlinda rais na kuhakikisha usalama wa sherehe ya uapishwaji.

Katuni ya Gado, iliyotolewa tarehe 1 Novemba 2025, kwenye akaunti yake ya Instagram. https://www.instagram.com/p/DQlMMdtjG97/utm_source=ig_web_copy_link&igsh=MzRlODBiNWFlZA==

Gado (jina lake halisi ni Godfrey Mwampemba), mchora-katuni ambaye ni Mtanzania na ambaye amekua akiishi Nairobi kwa miaka mingi, anajulikana sana kwa michoro yake makali ya maisha ya kisiasa ya Afrika Mashariki.[1] Katika katuni hii, alichora vipengele muhimu vya uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 2025, ambavyo vinadhihirisha waziwazi hofu ya ukandamizaji uliofanyika na kuharibu heshima ya Samia Suluhu Hassan. Aliweka katuni hii kwenye akaunti yake ya Instagram siku ya Jumamosi, Novemba 1, siku tatu tu baada ya uchaguzi uliofanyika Jumatano, Oktoba 29. Novemba 1 ilikuwa siku ambayo Tume ya Uchaguzi ilitangaza rasmi ushindi wa Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi wa urais wa Tanzania. Gado alitoa katuni hii bila kusubiri sherehe rasmi ya uapishwaji, ambayo iliandaliwa kwa haraka na kufanyika siku mbili baadaye, asubuhi ya Jumatatu, Novemba 3, mjini Dodoma.[2] Kwa hivyo, si taswira ya sherehe yenyewe ya uapishwaji, bali ni mchoro uliotoa ubashiri na uliolenga kueleza, ukweli halisi wa tukio hilo na aibu ya uapishwaji wa urais ulioandamana na ukandamizaji na kifo.

Ili kuelewa katuni ya Gado, tunahitaji kuangalia katuni hiyo katika muktadha wa matukio yanayoonyeshwa ndani ya siku tatu kuanzia siku ya uchaguzi hadi kutangazwa kwa matokeo. Ilikuwa kipindi cha hofu, wasiwasi, na uhaba wa taarifa, huku vituo vya kupigia kura vikiachwa tupu na maandamano yakianza siku ya uchaguzi katika miji mikuu ya Tanzania na kuendelea hadi matokeo yalipotangazwa. Pia ilikuwa kipindi cha ukandamizaji mkali dhidi ya vijana walioandamana, lakini kiwango cha ukandamizaji huu ulifichwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya kuzimwa kwa intaneti, mitandao ya kijamii, na simu za kimataifa (Minde, 2025). Kuzimwa huku kulianza alasiri ya tarehe 29 Oktoba na kukaendelea kwa wiki moja, na zuio la kutotoka nje liliwekwa Dar es Salaam, mji mkuu wa kibiashara wa nchi. Mawasiliano ya baharini kati ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani (yaani, Zanzibar) yalisitishwa na safiri za kimataifa zilitatizwa. Gado, ambaye anaishi Nairobi na hakuwa Tanzania wakati wa siku hizi za hofu, alipata taarifa hasa kwa njia ya simu, na, ingawa zilikuwa za vipande vipande, alielewa kwamba ghasia zilikuwa kali na waathiriwa walikuwa wengi[3].

Uchambuzi huu, ambao unachukulia uchoraji wa katuni za kisiasa kwa uzito (Limb & Olaniyan, 2018; Lent, 2009) na unalenga kuelewa ni nini kinaweza na nini hakiwezi kuchorwa, na kwa namna gani, katika muda mfupi uliojaa sintofahamu na mshtuko, unategemea mtazamo mpana zaidi kuhusu uchaguzi mkuu na maandamano yaliyoambatana nayo. Hata hivyo, muhtasari huo bado si kamili, kwani taarifa sahihi na zilizothibitishwa bado zinakosekana, kama ilivyo mtazamo unaohitajika kwa uchambuzi thabiti na usio na upendeleo wa mfululizo wa uchaguzi wa kushangaza—ambao hata hivyo masharti yake yalikuwa yamewekwa—katika nchi inayojivunia “amani na utulivu” wake, hasa wakati wa uchaguzi. Hadi sasa, utawala ulio madarakani umekuwa ukitumia aina ya utawala wa kiimla na unaotegemea “mifumo iliyojengeka vyema inayochanganya udhibiti wa taasisi, udhibiti wa polisi na vikosi vya usalama, desturi za muda mrefu za upendeleo wa kisiasa, ushawishi na uhisani (evergetism), na matumizi ya mbinu za jadi za utaifa wa kitanzania” (Maingraud-Martinaud & Fouéré, 2015, p. 145).

Mchoro wa Gado hivyo unaibua maswali yafuatayo: Je, tukio hili la ukandamizaji la mwaka 2025, lililoambatana na vifo vya mamia na maelfu ya watu, ni la kipekee, au, kinyume chake, ni ishara ya kuanzishwa kwa utawala wa kiimla, hata “udikteta” unaotegemea nguvu kali (Collord, 2025)? Na kwa nini, mwaka 2025, utawala haukuweza—au ulishindwa—“kuhakikisha muendelezo wa utawala wake wenyewe bila mtikisiko mkubwa, kwa ujanja na ufanisi” (Maingraud-Martinaud & Fouéré, 2015, p.145), kama ulivyofanikiwa kufanya tangu uhuru wa nchi? Kiini cha maandamano na ukandamizaji wa Oktoba 2025 ni mdororo wa uchumi wa maadili (moral economy)[4] chini ya shinikizo kutoka kwa watu wa tabaka la juu (elites) wenye tabia ya kiimla na uanyonyaji ambao wamesaliti sehemu kubwa ya jamii ya Tanzania.

Mkazo wa 1: Miili iliyorundikana chini ya zulia la sherehe

Mabaki ya waandamanaji wengi waliouliwa kuanzia mchana wa siku ya kupiga kura hadi sherehe ya uapisho tarehe 3 Novemba, na pengine siku nyingine zijazo, yamerundikana chini ya zulia ikiwa imefichwa lakini si sana. Ukatili uliofanywa ulilenga vijana wa kitanzania walioandamana kwa idadi kubwa katika mitaa ya miji mikuu ya Tanzania[5]. Picha na video zilizotangazwa nje ya Tanzania mara tu intaneti iliporejeshwa, baada ya kukatwa kwa wiki moja, zilionyesha kuwa wengi walioandamana walikuwa vijana wakiume—wakipinga uchaguzi wa udanginyifu na wakitaka CCM iondoke (Chama cha Mapinduzi), yaani chama tawala tangu uhuru wa taifa hilo. Walipataza sauti wakisema: “Hatutaki CCM,” “Tumechoka na CCM.” Lakini katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha, waandamanaji walipigwa risasi za moto na kuuawa. Wengine walipigwa, kujeruhiwa, au kudhalilishwa, kwa mfano, kulazimishwa kutambaa ardhini chini ya vitishio vya marungu na silaha za moto.

Kauli mbiu za waandamanaji pamoja na uharibifu na uchomaji wa maeneo maalum, kama vile vituo vya mafuta na mabasi ya masafa marefu yanavyomilikiwa na wanasiasa ambao pia ni wafanyabiashara wanaotuhumiwa kwa ufisadi, ni ushahidi zinaonyesha kwamba nyuma ya Samia Suluhu Hassan, kulikuwa na mfumo mzima uliokita mizizi, mfumo wa “chama-dola” (Makulilo, 2008), ulikuwa unakashifiwa. Chama-dola hiki, ambacho kiliridhi mfumo wa utawala wa chama kimoja nchini Tanzania kati ya mwaka 1964 na 1995, kinatuhumiwa kuanzisha mfumo wa vyama vingi ambao ni geresha tu. Vijana wa Tanzania walipotangaza kwamba hawakitaki tena chama cha CCM, bila shaka walikuwa wakitoa madai ya hali ngumu ya maisha na pia kukemea utekaji wa kimabavu wa demokrasia ya uchaguzi. Wapinzani wakuu wa Samia Suluhu Hassan walizuiwa kugombea uraisi kupitia mbinu mbalimbali: kuondolewa kwa visingizio vya kukosa nyaraka, kutekwa na kupotezwa, kupewa vitisho na kuteswa na hata kufikishwa mahakamani kwa tuhuma ya uhaini. Hasa, Tundu Lissu[6], kiongozi wa chama cha Chadema (Chama cha Demokrasia na Maendeleo) tangu Januari 2025. Lissu alipata umaarufu mkubwa kwa uwazi wake wa kusema bila uwoga na kudai usafi wa kisiasa dhidi ya ufisafi na matabaka ya wanyonyaji. Wakati wa uchaguzi, pia kulikua na tuhuma za wizi wa kura (kwa kujaza kura bandia kwenye masanduku ya kura), huku waandamanaji wakizuia mabasi madogo yaliyokuwa yakisafirisha kura zilizokwisha kujazwa.

Siku ya Jumamosi, tarehe 1 Novemba, Tume ya Uchaguzi ilipotangaza ushindi wa Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi wa urais wa Tanzania kwa asilimia 98 ya kura na ushiriki wa asilimia 85, jumuiya ya kimataifa ilipokea taarifa hiyo kwa mshangao. Hata hivyo, matokeo haya hayakuwashangaza wengi nchini Tanzania, ambako ilijulikana wazi kwamba uchaguzi huo ulishawatenga upinzani na kwamba idadi kubwa ya wapiga kura walisusia uchaguzi, licha ya ubabe wa CCM kwenye uchaguzi tangu kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi katikati ya miaka ya 1990[7]. Lakini kiini cha katuni ya Gado si fedheha ya ushindi wa (uongo wa) uchaguzi—yaani, uchaguzi uliopangwa au kuibwa—jambo ambalo si geni nchini Tanzania, wala hata si ile asilimia 98 ya kutia aibu, dharau ya wazi kwa wazo la mfumo wa vyama vingi. Badala yake, kinachoangaziwa ni ukatili, umwagaji damu, na upofu wa mbinu zilizotumika kufanikisha ushindi huo. Licha ya kwamba taarifa kuhusu ukubwa wa ukandamizaji zilikuwa bado hazijakamilika, Gado alitambua kuwa hali hiyo haikuwahi kushuhudiwa katika historia ya Tanzania huru. Pia alitabiri kwamba Samia Suluhu Hassan angepuuza kwa dharau mauaji yaliyofanyika—ambayo zulia katika katuni linaashiria. Mnamo Novemba 3, siku ya kuapishwa kwa rais mteule, wakati vyombo vikuu vya habari viliporipoti takriban vifo 50, wapinzani na wanaharakati wa haki za binadamu walitaja takwimu za vifo 3,000—ilipanda hadi 4,000 siku chache baadaye, jambo linaloelezea matumizi ya neno “mauaji ya halaiki” kuanzaa kutumika.[8] Kuanzia wakati huo, taarifa zilianza kuibuka kuhusu hatua zilizochukuliwa kuficha miili. Kulikuwa na ripoti za watu waliovaa barakoa kuvamia hospitali ili kuwamalizia majeruhi na kwenda kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti vilivyojaa kupita kiasi kuchukua miili, kupatikiana kwa makaburi ya halaiki na vilevile kufanyika kwa uchomaji wa siri wa maiti. Mnamo tarehe 6 Novemba, Gado alichapisha katuni mpya iliyolenga makaburi haya ya umati (https://www.instagram.com/freedomcartoonists/p/DR44yXziFGx/), ikionyesha hofu za familia za waliopoteza ndugu zao na mashirika ya kitaifa na kimataifa ya haki za binadamu wakilaani ukatili uliofanywa kufuatia matukio hayo.

Mkazo wa 2: “Mimi Samia Suluhu Hassan…”

 

 

Katika katuni yake ya tarehe 1 Novemba, Gado anamkosoa vikali Samia Suluhu Hassan kwa kuandaa kwa haraka sherehe ya kuapishwa, huku mikono yake ikiwa bado imechafuliwa na damu, siku mbili tu baada ya kutangazwa kwa ushindi wake na wakati ukandamizaji ukiendelea. Haraka hii ina maana kubwa: Katiba ya Tanzania inapiga marufuku kupinga matokeo ya uchaguzi kupitia njia za kisheria mara tu rais mpya anapoapishwa. Hivyo, ilikuwa lazima kuchukua hatua kwa haraka, huku wakizuia umati wa watu usivuruge sherehe hiyo au hata kutishia chama tawala. Hatari ya mapinduzi ilitanda katika kipindi chote cha uchaguzi na ilihitaji kuzuiwa. Wiki chache kabla ya uchaguzi, mtu aliyejitambulisha kama “Kapteni Tesha” alidai kuwa anatoka kikosi cha jeshi la anga na alitoa tamko akishutumu serikali kwa ufisadi na kuingilia siasa ndani ya jeshi. Katika video iliyosambazwa, aliwahimiza wananchi kuandamana na kudai haki zao (Lasteck, 2025). Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, hafla ya kuapishwa kwa rais haikufanyika katika uwanja wa michezo ulio wazi kwa umma na wenye uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya wananchi. Badala yake, ilifanyika kwa siri, kwa mwaliko maalum tu, katika makao ya kijeshi ya Dodoma, mji mkuu wa Tanzania—jiji ambalo kwa kiasi kikubwa huwa halina watu wengi ukiondoa nyakati muhimu za shughuli za kisiasa za kitaasisi (mji wa shamrashamra za nchi ukiwa Dar es Salaam).

Ikiwa fedheha ya Samia Suluhu Hassan imo katika haraka ya kuapishwa kwake, katika njia ya kificho ambayo hafla hiyo iliandaliwa, na dharau kwa waathiriwa, basi pia imo—kama Gado anavyodokeza—katika kufuru ya kidini: damu haikuchafua tu mikono ya Samia Suluhu Hassan, bali pia ilitia doa ushungi wake na kuikufuru Qur’ani anayoishika kwa mkono wake wa kulia wakati wa kuapishwa. Siku iliyofuata baada ya kuapishwa, ikiakisi katuni hiyo, ukurasa wa mbele wa gazeti la The Standard, gazeti la kila siku la Kenya lenye msimamo mkali wa ukosoaji, ulimwonyesha Samia Suluhu Hassan akiapa madarakani mbele ya mandhari ya moto, ukiwa na kichwa cha habari: “A bloody crown.” [Taji la damu][9] Inaonekana kama ni muda mrefu umepita tangu, akiwa Makamu wa Rais wa Tanzania, alipomrithi John Magufuli, aliyefariki mwezi Machi 2021, na kujipatia jina la upendo la “Mama Samia” kwa mtindo wa uongozi ulioonekana kuheshimu zaidi uhuru wa kiraia na kisiasa.

Je, sehemu ya Samia Suluhu Hassan katika katuni ya Gado, ambayo pia inaendana na taarifa za vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu hali ya Tanzania, inaakisi kwa usahihi jukumu lake katika kipindi hiki cha uchaguzi? Swali hili bado ni muhimu, huku sababu za ukatili zilizowakumba waandamanaji hazijawekwa wazi[10]. Inawezekana kuangalia historia ya kisiasa ya Samia Suluhu Hassan ili kutafuta sababu za mgeuko kuelekea utawala wa kibabe na kimabavu wenye ukandamizaji na umwagaji damu. Safari yake ya kisiasa ilianza Zanzibar ndani ya CCM; baadaye alipanda ngazi na kuwa Mbunge wa jimbo lake (anatoka Makunduchi, kusini mwa kisiwa cha Unguja) katika Bunge la Tanzania, kisha akawa Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Muungano. Tafsiri za kisaikolojia zinadhihirisha athari mbaya za ubaguzi na udhalilishaji alizoweza kukumbana nazo kama mwanamke katika ulimwengu wa wanaume wenye misimamo mikali na uchu wa madaraka, hasa baada ya kuwa Makamu wa Rais mwaka 2015. Ingawa mitazamo hiyo inastahili kuchukuliwa kwa uzito, ni muhimu kuihusisha na mienendo ya ndani ya dola-chama kama uwanja wa mapambano na vita vya makundi ya chama, ambayo huchangia pakubwa katika matumizi ya madaraka—ikiwa ni pamoja na michezo ya ushawishi inayohusisha si wanasiasa pekee, bali pia maafisa wa juu wa vyombo vya dola wanaounda mfumo wa chama-dola nchini Tanzania.

Kwa maneno mengine, licha ya urais wenye nguvu uliowekwa katika Katiba ambayo haijabadilishwa tangu 1977, ni lazima kufungua “sanduku jeusi” (blackbox) la jinsi maamuzi yanavyofanyika na yaliyosababisha ukandamizaji wa mwaka 2025 kwa kutazama zaidi ya Samia Suluhu Hassan na kujiuliza: Je, kundi la watu wake wa karibu lilichukua nafasi gani, wakiwemo mwanawe Abdul Hafidh Ameir, anayedaiwa kuunda kikosi binafsi cha wanamgambo kwa ajili ya kumhudumia mama yake, pamoja na vigogo kadhaa kutoka mtandao wa kisiasa-kiuchumi uliotokea Zanzibar—akiwemo mshauri wake wa karibu, Waziri Salum Rajabu, na mshauri wake binafsi, Haji Omar Kheir (Chachage, 2025; Chahali , 2025)? Je, kundi ndani ya CCM lililomuunga mkono na kumlinda Samia Suluhu Hassan, likiongozwa na rais wa zamani Jakaya Kikwete—mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za kitaifa—lilikuwa na nguvu kiasi gani? Vipindi viwili vya Kikwete madarakani, kuanzia 2005 hadi 2015, viligubikwa na kashfa kubwa zaidi za ufisadi kuwahi kushuhudiwa nchini Tanzania. Vipi kuhusu watu wenye nguvu ndani ya jeshi na, zaidi ya hapo, ndani ya jeshi la polisi? Na hatimaye, vipi kuhusu wahusika wa kigeni na wa kikanda? Maswali haya yanaturudisha kwenye kipengele cha tatu chenye uzito katika katuni ya Gado.

Mkazo wa 3: Wanaume wenye silaha, wakiwa wamevaa barakoa na wasiotambulika

Wanaume wenye silaha, wanaotisha, wakiwa wamevaa bereti, skafu na wakiwa wamevaa miwani za giza kuficha nyuso zao, wanasimama pembeni na kusimamia sherere ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan. Pia, kama Gado anavyoeleza mwenyewe[11], hao ndio waliokuwa wakisimamia ukandamizaji wa kikatili hapo awali. Na ni wao pia ambao, kama inavyoonyeshwa katika katuni ya tarehe 6 Novemba, walilinda operesheni zilizolenga kuondoa na kuficha miili ya waliouawa. Haikuwezekana kujua hawa watu ni nani kati ya siku ya kupiga kura na kutangazwa kwa matokeo, ndiyo maana Gado aliwachora wakiwa wamevaa sare za kijeshi nyeusi, na kuwafanya wasitambulike. Je, ni vikosi vya polisi vya Tanzania? Wanajeshi? Au ni wanamgambo? Je, ni Watanzania au wanatoka kwingineko? Taarifa zilizovuja wakati wa siku za ukandamizaji mkali zinatoa vidokezo fulani.

Kwanza, sehemu ya jeshi inadaiwa kuwa iliwaunga mkono waandamanaji na kujaribu kuwalinda vijana waliomiminika mitaani, bila kujiunga nao kikamilifu au kugeuza maandamano hayo kuwa jaribio la kutaka kuipindua serikali au kufanya mapinduzi. Matukio ya awali yaliyoonekana wakati wa maandamano yalionyesha wanajeshi wakitembea bega kwa bega kwa fahari pamoja na waandamanaji.[12] Pili, inaonekana kwamba maafisa wa polisi, badala ya jeshi, ndio waliokuwa wahusika wakuu wa vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya raia waliokuwa wakiandamana. Tangu mapema Novemba, maafisa wa polisi—wanaojulikana kuwa watekelezaji wa kazi chafu za chama tawala—walitajwa na kutambuliwa na mashirika ya kiraia na ya haki za binadamu kwa madai ya kuhusika kwao katika ukandamizaji huo. Orodha ya “Watu 100 Hatari zaidi Tanzania,” wakiitwa pia “wauaji,” “watekaji,” na “wafiraji,” ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii takriban siku kumi baada ya kuapishwa kwa rais, ikirudia orodha iliyowasilishwa katika ombi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na muungano wa mashirika ya kiraia na ya utetezi wa kisheria uliotaka uchunguzi wa uhalifu uliotendwa wakati wa uchaguzi uliopita. Hatimaye, siku moja baada ya uchaguzi, taarifa zilianza kusambaa zikidai kuwa baadhi ya waliotekeleza ukandamizaji hawakuwa Watanzania bali raia wa kigeni, huku ikirudiwa dhana kwamba nchi ya jirani ya Uganda ilituma wanajeshi kusaidia askari wa Tanzania. Huku uchaguzi mkuu wa Uganda ukikaribia katikati ya Januari 2026, iliripotiwa kwamba kuanguka kwa utawala wa Tanzania hakupaswi kuwa chanzo cha hamasa kwa vijana wa Uganda, huku Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 81 akijiandaa kugombea muhula mwingine baada ya miaka 40 ya utawala wa kimabavu na wa ukandamizaji.

Tunaweza sema kuwa ilikuwa hatari kubwa sana kuingia mitaani na kuandamana, kwa sababu sasa inaonekana wazi kuwa mwitikio mkali wa ukandamizaji kutoka kwa utawala ulikuwa umeandaliwa mapema, na hayakuwa matokeo ya tukio la ghafla achilia mbali jambo la bahati mbaya, kama wachambuzi wengine walivyodai. Hata hivyo, hoja inaweza kutolewa kwamba kiwango cha juu cha mauaji kilichoshuhudiwa kinaweza kwa sehemu kuelezwa na utambulisho wa wahusika waliotumika kukandamiza maandamano—yaani, maafisa wa usalama wasiozingatia sheria na wanamgambo kwa upande mmoja, na watu wasio Watanzania kwa upande mwingine. Kulikuwa na maonyo yaliyotolewa mara kwa mara wakati wa kampeni ya uchaguzi na Samia Suluhu Hassan pamoja na maafisa wa juu wa vyombo vya usalama, waliotilia mkazo kwamba maandamano kama hayo hayangeruhusiwa, yanaonekana kuwa yaliambatana na maandalizi madhubuti ya ukandamizaji huo mapema—lakini utaratibu halisi wa utekelezaji wake bado unahitaji kuchunguzwa. Je, mapinduzi yangewezekana kufanyika au tayari yalikuwa yameshaanza? Je, maandamano makubwa zaidi yangewezekana? Na tawala za kimabavu za nchi jirani za Uganda na Kenya zilitoa msaada gani? Swali hili lina maana sana ukizingatia kile kinachoitwa “udugu wa kimamamlaka” (fraternity of power) [13] au “mshikamano wa kimabavu” (authoritarian solidarity)[14] katika ngazi ya kikanda, ambao unalenga hasa wanaharakati wa haki za binadamu na harakati za maandamano? Maswali haya bado hayajajibiwa huku jamii ya Tanzania ikiendelea kuomboleza, ikidai haki kwa waliopoteza maisha, na ikitafuta kurejea katika hali ya kawaida. Tarehe 9 Desemba, siku ya maadhimisho ya Uhuru, wakati wanaharakati walipotoa wito wa kuandamana, mitaa ya Dar es Salaam ilibaki tupu kabisa.

Mfululizo huu wa makala ya Mambo! unajikita katika kuelezea mwaka wa uchaguzi wa 2025 nchini Tanzania. Unatoa maelezo ya kipekee wa usomaji wa kina na ukaribu wa vielelezo vya matukio ya kisiasa ya mwaka huu wa uchaguzi, uliokua na matukio mengi na uliotawaliwa na muendelezo wa ukandamizaji wa serikali. Katika kila sehemu cha mfululizo huu, tukio lililochaguliwa linazalishwa tena katika asili yake na kutafsiriwa panapohitajika, likiwekwa katika muktadha kwa uangalifu na kufafanuliwa au kupewa maelezo ya karibu kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa kuelewa kwa kina sehemu lilipotokea pamoja na maana na umuhimu wake. Matukio haya ni vyanzo ama nyaraka ya maana kwa ajili ya kuchambua muendelezo wa utawala wa kimabavu na ukandamizaji wa wazi uliofanywa na serikali ya Tanzania katika kipindi hiki cha uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2025.

Marejeleo

Cheeseman, N., Lynch, G., & Willis, J. (2020). The moral economy of elections in Africa. Democracy, voting and virtue. Cambridge University Press.

Chachage, C. (2025, November 8). Tragic October 29: Tanzania’s turning point? The Chanzo. https://thechanzo.com/2025/11/08/tragic-october-29-tanzanias-turning-point/

Chahali, E. (2025, November 20). Intelligence profile of Haji Omar Kheir: Presidential adviser during Tanzania’s ongoing post-election massacre with three decades of Zanzibar violence allegations against him. Ujasusi Blog. https://www.ujasusi.com/p/haji-omar-kheir-tanzania-presidential-adviser-massacre-allegations

Collord, M. (2025, November 4). After the coronation. Africa is a Country. https://africasacountry.com/2025/11/after-the-coronation

Gado (2012). Crisis…? What crisis?!@2005-2012. A Collection of Gado’s editorial cartoons, published in the Daily Nation, the Sunday Nation and the EastAfrican from 2005 to 2011. Buni Media.

Gado (2018). Gado (Godfrey Mwampembwa, Kenya/Tanzania). In P. Limb & T. Olaniyan (Eds.), Taking African cartoons seriously: Politics, satire, and culture (pp. 179-186). Michigan State University Press.

Lasteck, A. (2025, October 6). “Tanzania issues social media warning after video calls for military ‘action’.” BBC. https://www.bbc.com/news/articles/c62lj51kj2jo

Lent, J. A. (Ed.). Cartooning in Africa. Hampton Press.

Limb, P., & Olaniyan, T. (Eds.). 2018. Taking African cartoons seriously: Politics, satire, and culture. East Lansing: Michigan State University Press

Levitksy, S., & Way, L. (2010). Competitive authoritarianism: Hybrid regimes after the Cold War. Cambridge University Press.

Maingraud-Martinaud, C. & Fouéré, M.-A. (2015). Une hégémonie compétitive contre vents et marée : Les élections générales de 2015 en Tanzanie. Politique africaine 140(4), 145-163. https://doi.org/10.3917/polaf.140.0145

Makulilo, A. (2008). Tanzania: A de facto one party state? VDM Verlag.

Minde, N. (2025, November 5). Denied fair elections, Tanzanians make their mark through protests. ISS Today. https://issafrica.org/iss-today/denied-fair-elections-tanzanians-make-their-mark-through-protests

Morse, Y. L. (2014). Party matters: The institutional origins of competitive hegemony in Tanzania. Democratization, 21(4), 655-677. https://doi.org/10.1080/13510347.2013.764285

Riedl, R. B. (2014). Authoritarian origins of democratic party systems in Africa. Cambridge University Press.

Schedler, A. (2006). Electoral authoritarianism: The dynamics of unfree competition. Lynne Rienner Publishers.

Siméant, J. (2015). Three bodies of moral economy: The diffusion of a concept. Journal of Global Ethics, 11(2):163-175. DOI: 10.1080/17449626.2015.1054559 (Originally published as: Siméant, J. (2010). ‘Économie morale’ et protestation? Détours africains. Genèses, 81(4), 142-160).


Maelezo

[1] Angalia, kwa mfano, “Tanzanian Cartoonist Has a Stick for Every Powerful Eye,” The New York Times, Mei 1, 2020; “A true culture of editorial cartoons is developing throughout the region: Kenyan politicians under the fierce pen of Gado,” Le Monde, Juni 16, 2022; angalia pia Gado (2012, 2018).

[2] Tazama, katika mfululizo huu wa makala, kipindi cha 3 kuhusu hotuba ya Samia Hassan Suluhu katika sherehe yake ya uapishwaji kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

[3] Mahojiano na Gado, Novemba 6, 2025, Nairobi.

[4] Kuhusu matumizi ya dhana ya “uchumi wa kimaadili” (moral economy) katika masomo ya kiafrika (African studies), tazama hasa Siméant (2015). Kuhusu ufufuaji wake katika fikra kuhusu masuala ya uchaguzi barani Afrika, tazama Cheeseman et al. (2020).

[5] Kuna tofauti kati ya Tanzania Bara (inayolingana na eneo la Tanganyika ya zamani) na Tanzania Visiwani, yaani Zanzibar, kinachojumuisha hasa visiwa viwili vya Unguja na Pemba. Mnamo mwaka wa 2025, ni Tanzania bara pekee iliyoathiriwa na maandamano ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.

[6] Tundu Lissu ni mwanasheria na mwanachama wa chama cha Chadema, mkosoaji mkuu wa rais wa zamani John Magufuli (2015-2021) ambaye, mnamo 2017, alikuwa mwathirika wa jaribio la mauaji ambalo karibu alipoteza maisha yake. Tazama kipindi cha 1 cha mfululizo huu wa makala kuhusu hotuba ya Tundu Lissu kabla ya kukamatwa na kufungwa kwake gerezani mnamo Aprili 2025.

[7] Kuhusu utawala wa kidikteta wa uchaguzi na serikali mseto, tazama hasa Schedler 2006, Levitksy & Way (2010), na Riedl (2014). Kuhusu utawala wa nguvu mbadala wenye ushindani nchini Tanzania, tazama Morse (2014).

[8] Hali hii ilitokea wakati wa mjadala, “Kwenye Hatari ya Kupasuka: Ghasia za uchaguzi wa Tanzania wa 2025 na ukandamizaji unaozidi wa upinzani,” ulioandaliwa jioni ya tarehe 3 Novemba, 2025, kwenye X-Space na The Resistance Bureau, ukishirikisha hasa wanaharakati wa haki za binadamu wa Tanzania na Kenya.

[9] The Standard, “A Bloody Crown,” 4 Novemba 2025. Tazama, katika mfululizo huu wa makala, kipindi cha 4 kuhusu vichwa vya habari vya gazeti la kikenya la Standard wakati wa uchaguzi.

[10] Rais Samia Suluhu Hassan ameunda tume ya uchunguzi kuchunguza matukio yaliyofuata uchaguzi uliozua utata.

[11] Mahojiano na Gado, Novemba 6, 2025, Nairobi.

[12] Utafiti wa hivi karibuni wa Afrobarometer unaonyesha kuwa vijana wa kiafrika wanaona mapinduzi ya kijeshi kama njia mbadala kutokana na kukata tamaa kwa demokrasia na ufisadi ulioenea serikalini: https://www.afrobarometer.org/articles/young-africans-show-tolerance-for-military-intervention-a-wake-up-call-afrobarometer-ceo-tells-german-leaders/

[13] The Standard, November 4, 2025.

[14] BBC, “Are East African governments uniting to silence dissent?” June 27, 2025, https://www.bbc.com/news/articles/c4gk7435xl0o.


OpenEdition vous propose de citer ce billet de la manière suivante :
Marie-Aude Fouéré, Nicodemus Minde (4 mars 2026). Sehemu ya #2 Kuchora fedheha ya kimaadili ya Samia Suluhu Hassan: Katuni ya kisiasa ya Gado ya tarehe 1 Novemba 2025. Mambo ! Consulté le 16 avril 2026 à l’adresse https://doi.org/10.58079/15t4l


Vous aimerez aussi...

Laisser un commentaire

Votre adresse e-mail ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.