Sehemu ya #3 Miili ya kigeni, vijana waliopotoshwa: Hotuba ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan, 3 Novemba 2025
Nicodemus MINDE & Marie-Aude FOUÉRÉ, “Sehemu ya #3 Miili ya kigeni, vijana waliopotoshwa: Hotuba ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan, 3 Novemba 2025” Mambo! no. 108, 2026

Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wake rasmi kama Rais wa Jamhuri ya Tanzania, tarehe 3 Novemba, 2025 – Chamwino, Dodoma
Jumatatu tarehe 3 Novemba 2025, sherehe ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Tanzania ilifanyika katika uwanja wa gwaride la kijeshi mjini Dodoma, mji mkuu wa Tanzania, siku mbili tu baada ya ushindi wake kutangazwa. Mtandao wa intaneti, ambao ulikuwa umezimwa tangu siku ya kupiga kura (29 Oktoba), ulianza kurejeshwa katika hali yake ya kawaida taratibu. Tanzania ilikuwa imeanza kurejea katika hali yake ya kawaida baada ya kuwa gizani kwa wiki moja – ilikuwa kama kuzimu. Miaka minne kabla, tarehe 19 Machi 2021, Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais John Magufuli, hivyo akachukua wadhifa huo bila kuchaguliwa kupitia uchaguzi. Mwaka 2021, sauti ya uwazi ya Samia Suluhu Hassan iliakisi hisia za taifa: za huzuni na majonzi. Katika hotuba yake, aliliunganisha taifa lililokuwa linahitaji kufarijiwa na kuhakikishiwa kesho iliyo bora zaidi. “Sio siku nzuri kwangu kuongea nanyi kwa sababu nina kidonda moyoni. Leo nimeapa tofauti na wengine…nikiwa katika maombolezo,” alisema.
Na mwaka wa 2025, kama ilivyokuwa mwaka wa 2021, nchi pia ilikuwa katika maombolezo. Siku ya uchaguzi, vijana waliandaa maandamano kuonyesha kutoridhishwa kwao na mwelekeo wa nchi wa kuelekea utawala wa kidikteta (Paget, 2025). Muda mfupi baadae ukandamizaji wa kisiasa ulifuata. Wengi waliuawa; miili ya watu waliokufa ilitapakaa mitaani; vyumba vya kuhifadhia maiti zilijaa harufu kali ya miili iliyokuwa imekusanywa kwa wingi – hali hii ilikuwa ya mauaji ya kutisha. Wengine wengi waliteswa na kujeruhiwa vibaya. Watu walitafuta wapendwa wao bila mafanikio, huku ardhi ikiwa imelowa damu. Wapo pia waliochagua kunyamaza – si kwa sababu hawakuweza kuzungumza, bali kwasababu ilikuwa salama zaidi hivyo.
Hotuba ya uapisho ya Samia Suluhu Hassan ya mwaka 2025, ambayo tunaisoma kwa karibu kama nyenzo muhimu ya uchaguzi, inafanya kazi kama tendo la kisiasa ya ngazi ya juu (metapolitical act).[1] Hotuba hiyo inaelezea mchakato wa uchaguzi, inatoa tafsiri mbadala ya maandamano na vurugu zilizofuata, na inaangaliwa kupitia mtazamo wa serikali kama hatua ya kwanza ya kujihalalisha baada ya uchaguzi uliogubikwa na utata na vurugu. Lengo lake pia ni kuweka mwisho mchakato wa uchaguzi kama mwisho wa migogoro ya kisiasa. Hotuba hiyo inatumia sarufi maarufu ya amani, uzalendo (utanzania), na umoja, miongoni mwa zingine; dhana hizi zinatangulizwa mbele kama maadili ya uraia unaopaswa kuwa muhimu kuliko utata wa kisiasa. Hotuba halisi imechapishwa kwenye tovuti ya Ikulu ya taifa.[2] Kutokana na hotuba hiyo, tunaona jinsi matamshi ya kisiasa (speech acts) yanavyotumiwa kubadilisha tofauti za kisiasa na migogoro kuwa suala la kimaadili.
Kwa hivyo tunauliza: Hotuba ya uapisho ya Samia Suluhu Hassan inahalalishaje kuimarishwa kwa mamlaka ya kisiasa – kama si kuzama kwa nchi katika ukandamizaji na utawala wa kimabavu – kwa kuyawasilisha maandamano kama upotovu wa kimaadili, uingiliaji wa kigeni, au vurugu za kihalifu, huku kwa wakati huo huo ikisisitiza mada za umoja, maridhiano na na mazungumzo? Uchambuzi wetu umejikita katika utenaji wa matamshi (performativity) (Austin, 1975; Butler, 1997), umatini (textuality) (Barber, 2007), na utafiti kuhusu utawala wa kimabavu wa ushindani (competitive authoritarianism) (Levitsky & Way, 2010), ambazo zimeongoza vipindi vyetu viwili vilivyopita. Kwa kutegemea vifungu vilivyochaguliwa kutoka hotuba ya Samia Suluhu Hassan ya tarehe 3 Novemba, tunajaribu kuchambua na kujibu swali hili kupitia mada kadhaa: utaratibishaji wa uchaguzi (ritualization of elections); ugenishaji wa upinzani (foreignization of dissent), uhalalishaji wa dhana ya uhalifu kwa vijana (criminalization of youth) (yaani kudharau na kupuuza uhalai wa uwezo na uamuzi wa vijana); uhalalishaji wa kitaifa wa utaratibu kama suala la kimaadili (nationalistic moralization of order); kauli mbiu za mazungumzo na na maridhiano (rhetoric of dialogue and reconciliation); na mwisho, kupuuza kwa upole ripoti za waangalizi wa kimataifa.
Utaratibishaji wa uchaguzi – Mchakato hauna umuhimu
Pongezi zangu pia ziwaendee wote walioshinda kwenye nafasi za Ubunge;
Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi; na Udiwani kote nchini. Kwa wote niwaambie uchaguzi umekwisha, sasa tukafanye kazi ya kulijenga Taifa letu, na Utu wa Mtanzania.”
(…)
Ndugu zangu Watanzania, ni vyema tutambue kuwa uchaguzi mkuu wa Viongozi wa Serikali ni mchakato wa msimu mmoja tu ndani ya miaka mitano. Muda mwengine wote maisha lazima yaendelee. Hivyo basi, Jukumu letu sote kwa pamoja, ni kujenga nchi yetu na kuifanya kesho yetu iwe bora zaidi kuliko jana yetu. Niwasihi tuendelee kuilinda itikadi yetu ya umoja na mshikamano.
Tangu kuanza kwa mzunguko wa uchaguzi wa mwaka 2025, ujumbe mmoja ulikuwa wazi: chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) kingeshinda, na si kwa tofauti ndogo, bali kwa ushindi kubwa. Kulikuwa na hali ya kijiamini kupita kiasi katika mchakato wa uteuzi wa wagombea, kampeni, na maandalizi kwa ujumla. Kaulimbiu ya kampeni ya uhamasishaji ilikuwa Oktoba Tunatiki (yaani Oktoba tutapiga kura), ambayo ilikuwa kejeli kwa wito wa CHADEMA wa ‘Hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi’ (No reforms, no election). Wito huo wa kampeni uliweka mkazo katika kupiga kura kama ibada au desturi ya kisiasa badala ya utaratibu wa kidemokrasia wenye maana na wajibu wa kiraia ambamo maoni tofauti ya kisiasa yanajitokeza. Ulionyesha hisia ya kutokwepukika kwa matokeo, hata kwa wale ambao huenda wasingepiga kura kutokana na madai ya mageuzi; uliashiria kwamba uchaguzi ulikuwa tayari umeamuliwa mapema. Hii ilithibitisha kuwa ushindi wa uchaguzi umekuwa jambo la kawaida kama alama ya chama tawala. Mbali na kufungiwa kwa vyama vikuu vya upinzani – CHADEMA lakini pia Chama cha ACT-Wazalendo – kutoka kwenye uchaguzi wa urais, ilikuwa wazi kwamba CCM ilikuwa imedhamiria kushinda kwa gharama yoyote. Kutoka kwenye mikutano ya kampeni na vifaa vya kampeni vilivyotumika, CCM ilikuwa mbele sana kwa upande wa taswira na mwonekano. Nchi nzima ilijaa mabango ya Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza wake Emmanuel Nchimbi. Nchi nzima ilipambwa kwa rangi ya kijani na njano, ambazo ni rangi za chama. Pia ilikuwa wazi kwamba kampeni ilikuwa na ufadhili mkubwa. Mnamo Agosti 2025, miezi michache kabla ya uchaguzi, CCM ilifanya kampeni ya kuchangisha fedha na ikakusanya zaidi ya Tshs bilioni 86 (takriban Dola za Marekani milioni 32) (Wambura, 2025), huku michango mikubwa ikitoka katika sekta binafsi na za uchimbaji madini – ishara ya uhusiano wa karibu ndani ya mitandao ya watu wa juu (elites) katika uendeshaji wa chama na serikali (Gray, 2015; Morse, 2019). Hotuba ya uapisho ya Samia Suluhu Hassan ilisisitiza dhana ya uchaguzi kama ibada ya kisiasa inayofanyika kila baada ya miaka mitano badala ya kuwa mashindano la kweli na tkisiasa na kiraia linaloweza kuleta mabadiliko katika jamii.
Dhana ya kufungwa kwa mud awa kisiasa (temporal closure) – yaani, uchaguzi kama mwisho wa siasa – inaonekana wazi katika muktadha wa hotuba ya Samia Suluhu Hassan. Katiba ya Tanzania haina kifungu kinachoruhusu kupinga uchaguzi wa urais katika mahakama yoyote ya sheria. Muundo huu wa taasisi hubadilisha utangazaji wa matokeo ya uchaguzi kuwa kitendo kisichoweza kubatilishwa – yaani ukamilisho wa kikatiba. Hali hii inaeleza kwa nini uchambuzi mwingi wa vyombo vya habari na kisiasa ulisisitiza jinsi mchakato wa uchaguzi ulivyokuwa tu ibada ya kutawazwa (coronation ritual) (Collord, 2025) kwa chama kilichotawala kwa muda mrefu pamoja na rais wake. Upinzani ulikuwa umetaka marebisho katika kwenye tume ya uchaguzi, pamoja na mageuzi ya kikatiba na sheria ili kuwepo kwa mchakato wa kidemokrasia wenye ushindani wa kweli.
Ugenishaji wa Upinzani
Wote tunaoitakia mema nchi hii tumesikitishwa na kuhuzunishwa na matukio ya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha na uharibifu wa mali za Umma na mali za Watu binafsi kwenye baadhi ya maeneo nchini, hasa kwenye Majiji na Miji. Kilichotokea hakiendani na taswira na sifa za Kitanzania na sio Utanzania. Haikutushangaza kuona kuwa baadhi wa vijana waliokamatwa kutokana na kadhia hio wametoka nje ya Tanzania. Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vinaendelea kufuatilia na kuchunguza kwa undani zaidi kilichotokea, na kuirudisha nchi katika hali tuliyoizowea kwa haraka. Kamati ya Ulinzi ya Kitaifa, na Kamati za Ulinzi za Mikoa na Wilaya, hakikisheni kuanzia leo maisha ya Wananchi yanarejea mara moja. Pia nitumie fursa hii, kutoa onyo kwa wale wote waliochochea uvunjifu wa amani, na nawataka watambue kuwa vurugu na uvunjifu wa amani huishia kupimana nguvu na uwezo wa kujihami, ila mazungumzo huzaa mshikamano. Tuchague lenye manufaa kwetu, kwani usalama wa Taifa lolote hulindwa na wote kwa nguvu na gharama zozote.
Katika dondoo hii, Samia Suluhu Hassan anatumia hoja ya jadi ya uhuru wa taifa (sovereignty) ili kupunguza uhalali wa maandamano. Hotuba hii inaelezea upinzani kama jambo la kigeni na kama mbinu ya kuhalalisha hatua za serikali, hivyo basi ikihimiza vikosi vya usalama kuchunguza na kurudisha nchi katika hali yake ya kawaida. Mwezi Mei 2025, kundi la wanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kenya na Uganda walisafiri Kwenda Tanzania kutekeleza dhamira ya uangalizi wa kesi inayohusiana na kesi ya uhaini dhidi ya Tundu Lissu.[3] Baadhi ya wanaharakati walizuiwa katika uwanja wa ndege na kurejeshwa katika nchi zao. Miongoni mwa waliorejeshwa walikuwa aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya Willy Mutunga na Waziri wa zamani wa Masuala ya Katiba Martha Karua. Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi na Agather Atuhaire kutoka Uganda, ambao walifanikiwa kuingia nchini, baadaye walikamatwa, na kuripotiwa kuteswa kwao, na baadaye wakatupwa kwenye mipaka ya nchi zao husika (Amnesty International, 2025). Hivyo basi, kwa kulaumu maandamano kwa makundi ya kigeni, hotuba hiyo inaingiza wazo la ushawishi wa nje juu ya watu wanaowasilishwa kama wanaharibu uzalendo wa watu wa Tanzani, lakini kwa wakati huo huo wenye mtazamo finyu na wasioweza kuasi kwa kuwa wanathamini amani na utulivu. Anabainisha, hasa:
Kilichotokea hakiendani na taswira na sifa za Kitanzania na sio Utanzania. Haikutushangaza kuona kuwa baadhi wa vijana waliokamatwa kutokana na kadhia hio wametoka nje ya Tanzania.
Katika hotuba zilizofuata, alieleza zaidi kwamba vipengele vya kigeni vilikuwa na na mipango ya uovu ya kuleta vurugu na kuisambaratisha Tanzania (Mwakideu, 2025). Katika mazingira ya utawala wa kimabavu wa uchaguzi (electoral authoritarianism) (Schedler, 2006; Levitsky & Way, 2010), mkakati wa kuigenisha upinzani (foreignization) hutumika kupunguza uhalali wa upinzani wa ndani, kuhalalisha hatua za kiusalama, na kuimarisha hisia za kitaifa. Ingawa tunaweza kuitazama kauli hii kama kauli inayohusisha nchi nyingine, kuna njia nyingine ya kuigenisha upinzania ambayo inaweza kuhusisha Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania (diaspora). Diaspora ya Watanzania imekuwa ikiongeza sauti kuhusu kile wanachokiona kama kurudi nyuma kwa demokrasia na kuongezeka kwa utawala wa kimabavu nchini. Miongoni mwa wana-diaspora wa Tanzania ni Mange Kimambi, mwanamitindo aliyebadilika kuwa mwanaharakati. Mange Kimambi, anayeishi Marekani, ametumia majukwaa ya kidijitali—hasa Instagram, ambayo ni maarufu sana Tanzania—kukosoa chama tawala, CCM, na mitandao yake ya watu wa tabaka la juu. Wakati wa kipindi cha uchaguzi, Mange Kimambi alijiweka kama sauti ya kueneza na kukuza malalamiko ya Watanzania akiwa nje ya Tanzania. Baadaye alipewa onyo kwamba angekamatwa iwapo angeingia Tanzania, na angekabiliwa na mshatak ya kuchochea vurugu, kuhujumu uchumi na utakatishaji fedha.
Uwekaji wa vijana katika taswira ya uhalifu
Haikutushangaza kuona kuwa baadhi wa vijana waliokamatwa kutokana na kadhia hio wametoka nje ya Tanzania.
Vijana wanawekwa katika taswira, sio kama wapinzani halali wa kisiasa wanaostahili kusikilizwa, bali kama watu waliosababisha vurugu na uasi, walioathiriwa na wageni, na waliotishia umoja wa kitaifa. Samia Suluhu Hassan alidai kwamba baadhi ya vijana, kwa kusema kidogo, “wametoka nje ya Tanzania” – kauli iliyotafsiriwa kama jaribio la kupunguza au kudharau uwezo wa vijana wa Tanzania. Katika hotuba ya baadaye kwa wazee wa Dar es Salaam, ambapo umati uliokusanyika kumsikiliza rais akielezea matukio ya 29 Oktoba na siku zilizofuata, alizidi kudhoofisha uhalali wa maandamano hayo kwa kuyaelezea kama vurugu na yaliyopangwa kusababisha fujo (The Chanzo Reporter, 2025). Vijana wenye umri wa miaka 35 au chini wanaunda takriban asilimia 77 ya idadi ya watu nchini Tanzania. Zaidi ya asilimia 50 ya idadi ya wananchi wako chini ya ya umri wa miaka 18, huku umri wa wastani ukiwa kati ya miaka 17-17.6, jambo linaloakisi idadi ya watu ambao ni vijana. Kama wenzao barani Afrika, vijana wanakabiliwa na changamoto kama vile ukosefu wa ajira na kutengwa kisiasa. Uamuzi wa kuandamana siku ya uchaguzi unaakisi kukata tamaa kwao na jinsi uchumi unavyoendeshwa, ukosefu wao wa imani katika taasisi za kisiasa, Pamoja na ubadhirifu wa fedha za umma. Hta hivyo, hotuba ya uapisho haikukiri malalamiko haya hata kidogo, na badala yake inawaonyesha vijana kama wasio kuwa na madai halali. Katika hotuba nyingine, wakati huu katika ufunguzi rasmi wa Bunge tarehe Novemba 14, 2025, Samia Suluhu Hassan alitumia msemo “wanafuta mkumbo” (ikimaanisha, wanafuata umati; wanatenda kwa mtazamo wa kundi) kwa namna ya balagha (rhetoric), na kwa njia ya dharau, kupunguza uwezo wa vijana kujitambua na kufanya maamuzi yao wenyewe kisiasa. Kwa kifupi, vijana waliandamana bila kufikiri. Hii inaimarisha tofauti ya kizazi na kuhalalisha mauaji yaliyofuata baada ya maandamano. Vijana pia walielezwa kama sio wazalendo: Kile kilichotokea, kwa mtazamo wake, hakiendani na taswira na tabia ya Watanzania na si la Kitanzania. Anasistiza dhana Fulani ya maana ya kuwa “Mtanzania” ambayo inaendana na simulizi kuu ya utaifa wa Tanzania tangu uhuru, lakini pia ni dhana ya kudumisha utawala wa kiimla na unyonyaji wa viongozi wa tabaka la juu kwa kukanusha na kuzima maono mbadala ya jinsi siasa na jamii zinavyopaswa kuendeshwa.
Uhalalishaji wa nidhamu ya kitaifa kwa hoja za kimaadili
Ili tuweze kuyatimiza hayo, hatuna budi kuhakikisha tunahimizana umoja na upendo kwa nchi yetu, tunadumisha amani na kuheshimu sheria za nchi. Kinyume cha hayo, Maandamano, vurugu na uvunjifu wa amani, husababisha maumivu na havileti manufaa wala faida kwa yeyote. Niwasihi Watanzania tuchague hekima badala ya ghadhabu; busara badala ya mihemuko; upendo badala ya chuki; uvumilivu badala ya vinyongo; umoja badala ya mgawanyiko; amani badala ya vurugu; unyenyekevu badala la kiburi; na huruma badala ya hasira.”
(…)
Nimeamua kutumia jukwaa hili leo kushukuru na kupongeza kwa kumaliza uchaguzi, kuhimiza Umoja na Mshikamano wa Kitaifa na kusisitiza kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Taifa ni muhimu zaidi kuliko matakwa binafsi ya mtu yeyote. Masuala ya mwelekeo wa kazi za Serikali kwa miaka mitano ijayo, na ufafanuzi wa kina wa hatua zitakazochukuliwa kutekeleza dhana ya Kazi na Utu utatolewa katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hotuba hii inarudia tena lugha ile ile ya utaifa ili kuunda dhana ya taifa—Tanzania—na kuwasilisha taifa kama jamii yenye maadili. Matumizi ya mara kwa mara ya kauli kama “umoja na upendo wa nchi yetu” na “kujenga umoja na mshikamano wa taifa letu” yanalenga kuimarisha mtazamo unaotafsiri maandamano kama jambo la kigeni, huku yakifanya kazi kama mwito wa kizalendo wa kuhamasisha uzalendo miongooni mwa wananchi. Taifa la Tanzania linaonyeshwa si tu kama taasisi ya kisiasa bali pia kama yenye maadili. Kauli “Kilichotokea hakiendani na taswira na sifa za Kitanzania na sio Utanzania” inasisitiza mtazamo huu. Mara nyingi, serikali za kiimla huimarisha utaifa au kile wakosoaji wanachokiita utaifa bandia (pseudo nationalism) kwa kutumia utambulisho wa kitaifa kuhalalisha mamlaka yao (autocratic legitimation) (Dukalskis & Lee, 2020). Hivyo basi, Utanzania (kuwa Mtanzania), unawasilishwa kama sharti la kimaadili badala ya wajibu wa kiraia.
Lugha ya kisiasa ya mazungumzo na maridhiano
Kama mnavyofahamu, katika kuliunganisha Taifa, Serikali ya awamu ya sita tulianza na falsafa ya 4R’s, inayosimamia misingi ya kuzungumza na kuelewana (Reconciliation), kuvumiliana (Resilience), kubadilisha mwelekeo baada ya maelewano (Reforms) na kuendelea kujenga Taifa letu (Re Construction/Building). Tunapoendelea mbele hatutachoka wala kurudi nyuma kwenye kusimamia yote yanayohusu kujenga Umoja na Mshikamano wa Taifa letu.
Wakati Samia Suluhu Hassan alipomrithi Magufuli mwaka 2021, alijitambulisha kama kiongozi wa mageuzi, akiendeleza kile kilichoitwa falsafa ya 4R: Kuzungumza na kuelewana (reconciliation), Kuvumiliana (resilience), kubadilisha mwelekeo baada ya maelewano (reforms), na Kujenga taifa (reconstruction). Hata hivyo, Samia Suluhu Hassan alitumia ahadi, michakato, na ucheleweshaji kama mikakati ya kudhibiti matarajio ya wananchi, hata wakati ukandamizaji uliendelea (Paget & Kwayu, 2025). Katika mwaka wake wa kwanza kama rais, kwa kweli alionekana kuunga mkono falsafa hiyo. Hata hivyo, baadaye alianza kurudi nyuma na kuvunja ahadi zake. Kadiri nchi ilivyokaribia uchaguzi, watu wengi waliendelea kutoa wito wa maridhiano na mazungumzo ya kisiasa. Madai makuu yalihusisha mageuzi ya uchaguzi na ya taasisi za kisiasa. Madai haya yalitolewa na upinzani, hususan CHADEMA, ambayo ilichukua msimamo mkali zaidi: “No reforms, No elections.” Hatimaye, dola ilianza kuutazama msimamo huu kama uhaini. Katika kipindi cha uchaguzi, CCM mara kwa mara ilikataa wito wa maridhiano na mazungumzo, mara nyingi ikisisitiza kwa ujasiri kwamba mazungumzo yanaweza kufanyika tu baada ya uchaguzi. Kwa kuitaja falsafa ya 4R, hotuba hiyo inaendeleza mtazamo kwamba falsafa hiyo inatumika kwa maslahi ya kisiasa badala ya kutekelezwa kwa dhati. Tangu 29 October, dola haijachukua wajibu kwa vurugu na mauaji yaliyofuatia. Badala yake, kama inavyoonekana katika mada zinazojitokeza, lawama zimeelekezwa kwa wahusika wa nje na kwa vijana wanaowasilishwa kama kundi la waleta vurugu.
Kudunisha uhalali wa waangalizi wa kimataifa – kurejelewa kwa maandishi (intertextuality) na hotuba za Rais Mkapa
Kama kawaida, kwa nchi zenye mfumo wa Kidemokrasia hualika waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya za Kimataifa na Kikanda kuja kushuhudia mchakato wa uchaguzi. Uwepo wao huongeza uhalali wa juhudi zetu za kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwenye mazingira ya uwazi, haki, heshima na utawala wa sheria. Kwa muktadha huu, tunazishukuru Jumuiya zote zilizoleta waangalizi wa uchaguzi. Kutoka Afrika tulikuwa na waangalizi kutoka Umoja wa Afrika (AU); Jumuiya ya nchi za Maziwa Makuu (ICGLR); Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika (SADC); na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Pamoja na hao, tulikuwa na wengine kutoka maeneo mbalimbali. Makundi yote ya waangalizi yameshatoa taarifa za awali, na tunawashukuru kwa kuwa nasi, na kwa heshima kubwa tumepokea maoni yenu. Hata hivyo, kama alivyowahi kusema Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa mwaka 2000 wakati akiapishwa kuwa Rais, na hapa ninakinukuu kipande cha Hotuba hiyo, kinachosema ‘’nawashukuru watazamaji wa kimataifa kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika, walipotusifia tumepokea sifa hizo kwa unyenyekevu. Tumesikia pia waliyodhani hayakwenda sawa na mengine hata sisi tumeyaona. Maagizo yao tumeyakataa, ushauri wao tutauzingatia ili tufanye vizuri zaidi siku zijazo.
Kwa hakika, kama hotuba inavyoonyesha, makundi ya waangalizi wa uchaguzi tayari yalikuwa yametoa taarifa zao za awali kuhusu mwenendo wa uchaguzi nchini Tanzania kufikia wakati wa kuapishwa. Misheni kadhaa za waangalizi wa kimataifa na kikanda zilitoa tathmini kali kuhusu namna uchaguzi ulivyoendeshwa, si tu kutoka nchi za ukanda wa kaskazini (Global North) bali pia kutoka barani Afrika, hasa kutoka SADC. Hotuba hii inajielekeza kwa waangalizi wa kimataifa, ikitoa shukrani na kusisitiza kwamba uwepo wao unaongeza uhalali wa juhudi za kuendesha uchaguzi ulio wazi, wa haki, wa kuheshimu misingi ya sheria, na unaozingatia utawala wa sheria. Inayatambua pia makundi ya waangalizi kama AU, ICGLR, SADC, na EAC. Mrejeo muhimu wa kimatini katika hotuba hiyo unatokana na nukuu ya hotuba ya kuapishwa ya mwaka 2000 ya rais mstaafu Benjamin Mkapa.[4]
‘Nawashukuru pia watazamaji wa kimataifa kwa kuamua kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika. Walipotusifia tumepokea sifa hizo kwa unyenyekevu. Tumesikia pia wanayodhani hayakwenda saw ana mengine hata sisi tumeyaona. Maagizo yao tumeyakataa. Usharui wao tutauzingatia ili tufanye vizuri zaidi siku zijazo. Narudia. Usharui wao tutauzingatia ili tufanye vizuri zaidi siku zijazo. Tunawashukuru sana.’[5]
Hotuba hiyo inawashukuru waangalizi wa kimataifa kwa pongezi zao, inakiri kuwepo kwa mapungufu fulani, lakini inakataa “maelekezo” yao huku ikikubali “ushauri” wao. Mrejeo huu wa kimatini unafanya kazi kama onyesho la mamlaka ya kitaifa (sovereignty performance): unapata uhalali wake kwa kurejea kauli za marais waliotangulia na kubadilisha ukosoaji kuwa aina ya ushauri ambao dola inaweza kuupokea tu kwa masharti yake yenyewe.
Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Wakati wa Kuapishwa Kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tarehe 3 Novemba, 2025 – Chamwino, Dodoma
Habari ya asubuhi.
Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuturuzuku uhai na kutuwezesha kushiriki sherehe hizi za kihistoria kwa Taifa letu. Pili niwashukuru Watanzania wote kwa imani yao kwa Chama cha Mapinduzi, na kwa mapenzi
makubwa, na kutupa mimi na Makamu wa Rais fursa hii adhimu ya kuwatumikia.
Shukrani za kipekee kwa Viongozi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi, kwa namna walivyoendesha kampeni kwa mafanikio makubwa.
Niishukuru tena Tume ya Uchaguzi kwa kuratibu na kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi kwa ufanisi usiotiliwa shaka.
Ndugu Viongozi;
Ndugu Wananchi;
Katika Uchaguzi huu tulikuwa na wagombea 17 kutoka vyama mbalimbali vya siasa tukiwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda kuwashukuru wenzangu 17 ambao kwa hakika mmeonesha ukomavu wa kidemokrasia kwa kuendesha kampeni ambazo tulishindana kwa hoja, na sote tulionesha, kuwa siasa sio vita. Tumemaliza vyema uchaguzi na kumpongeza alieshinda.Aidha, nitumie fursa hii pia kumpongeza sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi na Vyama vya Siasa vilivyokuwa kwenye mchakato wa uchaguzi, kwa kumaliza uchaguzi kwa salama na amani. Zanzibar Oyeee!
Pongezi zangu pia ziwaendee wote walioshinda kwenye nafasi za Ubunge; Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi; na Udiwani kote nchini. Kwa wote niwaambie uchaguzi umekwisha, sasa tukafanye kazi ya kulijenga Taifa letu, na Utu wa Mtanzania.
Waheshimiwa Marais;
Viongozi;
Ndugu Wananchi;
Shughuli inakuwa nzuri na ya kufurahisha ikihudhuriwa na wanaokupenda. Tanzania leo imejawa na furaha kubwa kuona baadhi ya Waheshimiwa Marais wenzangu na viongozi mbalimbali wa nchi jirani wamejumuika nasi katika tukio hili, pamoja na kwamba tulitoa mwaliko kwa muda mfupi. Kwa wale walioshindwa kushiriki tunatambua uzito wa majukumu yao, na tunajua mioyo yao ipo pamoja nasi. Tunawashukuru pia wote waliotuma salamu za pongezi kwetu. Tunasema ahsanteni sana.
Ndugu Wananchi;
Uchaguzi ni fursa kwa Wananchi kueleza matakwa yao ya aina ya viongozi wanaodhani wataweza kuwatumikia vyema, na kuwaletea maendeleo endelevu. Kipindi cha kampeni tuligawika kiitikadi na kishabiki kama taifa. Ila baada ya uchaguzi kufanyika, anaechaguliwa na wengi huwa ndio chaguo la nchi na anapaswa kuwa Mtumishi wa Wananchi wote, waliomchagua, waliochagua wagombea wengine, na hata ambao hawakushiriki uchaguzi. Kwa sisi tuliochaguliwa, ahadi yetu ni kulitumikia Taifa hili kwa nguvu zetu zote, vipawa vyetu vyote na maarifa yetu yote.
Ndugu zangu Watanzania, ni vyema tutambue kuwa uchaguzi mkuu wa Viongozi wa Serikali ni mchakato wa msimu mmoja tu ndani ya miaka mitano. Muda mwengine wote maisha lazima yaendelee. Hivyo basi, Jukumu letu sote kwa pamoja, ni kujenga nchi yetu na kuifanya kesho yetu iwe bora zaidi kuliko jana yetu. Niwasihi tuendelee kuilinda itikadi yetu ya umoja na mshikamano.
Ndugu Wananchi;
Wote tunaoitakia mema nchi hii tumesikitishwa na kuhuzunishwa na matukio ya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha na uharibifu wa mali za Umma na mali za Watu binafsi kwenye baadhi ya maeneo nchini, hasa kwenye Majiji na Miji. Kilichotokea hakiendani na taswira na sifa za Kitanzania na sio Utanzania. Haikutushangaza kuona kuwa baadhi wa vijana waliokamatwa kutokana na kadhia hio wametoka nje ya Tanzania. Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vinaendelea kufuatilia na kuchunguza kwa undani zaidi kilichotokea, na kuirudisha nchi katika hali tuliyoizowea kwa haraka. Kamati ya Ulinzi ya Kitaifa, na Kamati za Ulinzi za Mikoa na Wilaya, hakikisheni kuanzia leo maisha ya Wananchi yanarejea mara moja. Pia nitumie fursa hii, kutoa onyo kwa wale wote waliochochea uvunjifu wa amani, na nawataka watambue kuwa vurugu na uvunjifu wa amani huishia kupimana nguvu na uwezo wa kujihami, ila mazungumzo huzaa mshikamano. Tuchague lenye manufaa kwetu, kwani usalama wa Taifa lolote hulindwa na wote kwa nguvu na gharama zozote.
Ndugu Viongozi;
Ndugu Wananchi;
Kama kawaida, kwa nchi zenye mfumo wa Kidemokrasia hualika waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya za Kimataifa na Kikanda kuja kushuhudia mchakato wa uchaguzi. Uwepo wao huongeza uhalali wa juhudi zetu za kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwenye mazingira ya uwazi, haki, heshima na utawala wa sheria. Kwa muktadha huu, tunazishukuru Jumuiya zote zilizoleta waangalizi wa uchaguzi. Kutoka Afrika tulikuwa na waangalizi kutoka Umoja wa Afrika (AU); Jumuiya ya nchi za Maziwa Makuu (ICGLR); Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika (SADC); na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Pamoja na hao, tulikuwa na wengine kutoka maeneo mbalimbali. Makundi yote ya waangalizi yameshatoa taarifa za awali, na tunawashukuru kwa kuwa nasi, na kwa heshima kubwa tumepokea maoni yenu. Hata hivyo, kama alivyowahi kusema Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa mwaka 2000 wakati akiapishwa kuwa Rais, na hapa ninakinukuu kipande cha Hotuba hiyo, kinachosema
‘nawashukuru watazamaji wa kimataifa kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika, walipotusifia tumepokea sifa hizo kwa unyenyekevu. Tumesikia pia waliyodhani hayakwenda sawa na mengine hata sisi tumeyaona. Maagizo yao tumeyakataa, ushauri wao tutauzingatia ili tufanye vizuri zaidi siku zijazo.’
Ndugu Wananchi;
Sifa moja ya Mwanadamu ni kutokukamilika, aliekamilika kabisa kabisa bila kasoro yoyote ni Mwenyezi Mungu peke yake. Ndio maana, katika shughuli au harakati za wanaadamu tunaunganishwa na mawasiliano, mazungumzo na maelewano, au kwa maneno mengine, tunaunganishwa na uwepo wa Suluhu ya mambo katika jamii zetu. Kama mnavyofahamu, katika kuliunganisha Taifa, Serikali ya awamu ya sita tulianza na falsafa ya 4R’s, inayosimamia misingi ya kuzungumza na kuelewana (Reconciliation), kuvumiliana (Resilience), kubadilisha mwelekeo baada ya maelewano (Reforms) na kuendelea kujenga Taifa letu (Re Construction/Building). Tunapoendelea mbele hatutachoka wala kurudi nyuma kwenye kusimamia yote yanayohusu kujenga Umoja na Mshikamano wa Taifa letu.
Ndungu Watanzania;
Mkusanyiko wetu leo hapa, sio kwa ajili ya kuzawadia walioshinda kwenye uchaguzi, la hasha; bali ni matakwa ya kikatiba ya kukabidhiwa dhamana ya kuwa mtumishi mkuu wa Taifa katika kuleta maendeleo endelevu; kwa maana ya uimara wa Kiuchumi, Kisiasa, kidiplomasia na Kijamii. Ili tuweze kuyatimiza hayo, hatuna budi kuhakikisha tunahimizana umoja na upendo kwa nchi yetu, tunadumisha amani na kuheshimu sheria za nchi. Kinyume cha hayo, Maandamano, vurugu na uvunjifu wa amani, husababisha maumivu na havileti manufaa wala faida kwa yeyote. Niwasihi Watanzania tuchague hekima badala ya ghadhabu; busara badala ya mihemuko; upendo badala ya chuki; uvumilivu badala ya vinyongo; umoja badala ya mgawanyiko; amani badala ya vurugu; unyenyekevu badala la kiburi; na huruma badala ya hasira. Taifa letu ni bora na lina nguvu zaidi kuliko mtu yeyote. Demokrasia haipimwi kwa nani kashinda uchaguzi, bali kwa jinsi tunavyoendesha mambo yetu baada ya uchaguzi. Tutakuwa na nguvu zaidi pale kila sauti, chanya na hasi, zinaposikilizwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa, na vile vile, tunapoweza kuponya penye maumivu. Hii si kazi ya upande mmoja wa Serikali peke yake, bali ni kwa kila Jumuiya za Wananchi, Chama cha Siasa, Dini zetu, na kila mwananchi. Na hapa, nitumie fursa hii, kuwashukuru kwa dhati ya moyo wangu Viongozi wa Dini waliohimiza amani na upendo katika kipindi chote cha uchaguzi.
Ndugu Wananchi;
Nimeamua kutumia jukwaa hili leo kushukuru na kupongeza kwa kumaliza uchaguzi, kuhimiza Umoja na Mshikamano wa Kitaifa na kusisitiza kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Taifa ni muhimu zaidi kuliko matakwa binafsi ya mtu yeyote. Masuala ya mwelekeo wa kazi za Serikali kwa miaka mitano ijayo, na ufafanuzi wa kina wa hatua zitakazochukuliwa kutekeleza dhana ya Kazi na Utu utatolewa katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya kusema hayo, niwashukuru wote kwa kujumuika nasi kwenye tukio hili muhimu na la kihistoria. Nimepokea pongezi zote kwa heshima kubwa, na sasa safari ya kuwatumikia Watanzania kwa kipindi cha pili inaanza rasmi.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Mungu Ibariki Afrika…!
Mungu Ibariki Tanzania…!
| Mfululizo huu wa makala ya Mambo! unajikita katika kuelezea mwaka wa uchaguzi wa 2025 nchini Tanzania. Unatoa maelezo ya kipekee wa usomaji wa kina na ukaribu wa vielelezo vya matukio ya kisiasa ya mwaka huu wa uchaguzi, uliokua na matukio mengi na uliotawaliwa na muendelezo wa ukandamizaji wa serikali. Katika kila sehemu cha mfululizo huu, tukio lililochaguliwa linazalishwa tena katika asili yake na kutafsiriwa panapohitajika, likiwekwa katika muktadha kwa uangalifu na kufafanuliwa au kupewa maelezo ya karibu kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa kuelewa kwa kina sehemu lilipotokea pamoja na maana na umuhimu wake. Matukio haya ni vyanzo ama nyaraka ya maana kwa ajili ya kuchambua muendelezo wa utawala wa kimabavu na ukandamizaji wa wazi uliofanywa na serikali ya Tanzania katika kipindi hiki cha uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2025. |
Marejeo
Amnesty International. (2025, May 23). Tanzania: Torture and forcible deportation of Kenyan and Ugandan activists must be urgently investigated. https://www.amnesty.org/en/latest/news/2025/05/tanzania-torture-and-forcible-deportation-of-kenyan-and-ugandan-activists-must-be-urgently-investigated/
Austin, J. L. (1975). How to do things with words. Harvard University Press.
Barber, K. (2007). The anthropology of texts, persons and publics. Cambridge University Press.
Bevir, M. (Ed.). (2010). Metapolitics. In Encyclopedia of political theory, Vol. 3, pp. 879–880. SAGE Publications, Inc. https://doi.org/10.4135/9781412958660.n282
Butler, J. (2021). Excitable speech: A politics of the performative. Routledge.
Dukalskis, A., & Lee, J. (2020). Everyday nationalism and authoritarian rule: A case study of North Korea. Nationalities Papers, 48(6), 1052–1068. doi:10.1017/nps.2019.99
Gray, H. S. (2015). The political economy of grand corruption in Tanzania. African Affairs, 114(456), 382–403.
Levitsky, S. & L. Way. (2010). Competitive authoritarianism: Hybrid regimes after the Cold War. Cambridge University Press.
Morse, Y. L. (2019). How autocrats compete: Parties, patrons, and unfair elections in Africa. Cambridge University Press.
Mwakideu, C. (2025, December 2). Samia on poll protests: “No way — we’d have done nothing”. The East African. https://www.theeastafrican.co.ke/tea/news/east-africa/samia-on-poll-protests-no-way-we-d-have-stood-done-nothing-5284676
Paget, D. (2025, November 1). Tanzania: President Samia Hassan’s grip on power has been shaken by unprecedented protests. The Conversation Africa. https://theconversation.com/tanzania-president-samia-hassans-grip-on-power-has-been-shaken-by-unprecedented-protests-268849
Paget, D., & Kwayu, A. C. (2025). Tanzania’s autocratic reform-washing. Journal of Democracy, 36(3), 78–91.
Schedler, A. (2006). Electoral authoritarianism: The dynamics of unfree competition. Lynne Rienner Publishers.
The Chanzo Reporter. (2025, December 3). ‘Yale Hayakuwa Maandamano’ : Hotuba Kamili ya Rais samia Akiongea na Wazee wa Dar es Salaam, Disemba 2, Kuhusiana na Matukio ya Okt. 29, 2025. The Chanzo. https://thechanzo.com/2025/12/03/yale-hayakuwa-maandamano-hotuba-kamili-ya-rais-samia-akiongea-na-wazee-wa-dar-es-salaam-disemba-2-kuhusiana-na-matukio-ya-okt-29-2025/
Wambura, B. (2025, August 13). Tanzanian tycoons, miners and leaders give CCM over Sh86 billion for 2025 campaign, party building. The Citizen. https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/tanzanian-tycoons-miners-and-leaders-give-ccm-over-sh86-billion-for-2025-campaign-party-building-5153100
Maelezo
[1] Metapolitiki inahusu uhusiano maalum kati ya siasa na fikra za kisiasa, iwe inatazamwa kwa mtazamo chanya au hasi. Uhusiano huu unaunganisha matukio ya siasa, utawala, na utungaji sera na vigezo vya kinadharia, historia ya kiakili, au falsafa
[2] Tazama https://share.google/Oe1eea8ybnRNBDggw; imezalishwa katika asili yake na kupatikana mwishoni mwa sehemu hii.
[3] Tazama sehemu ya 1 katika mfululizo huu “Hotuba ya Tundu Lissu ya tarehe 3 Aprili 2025, ‘Tutakinukisha: Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi’.”
[4] Rais Benjamin Mkapa alikuwa Rais wa Tanzania kati ya mwaka 1995-2000.
[5] Tazama hotuba kamili ya ufunguzi ya Rais Benjamin Mkapa hapa: https://www.youtube.com/watch?v=K5jJIV3iAE0
OpenEdition vous propose de citer ce billet de la manière suivante :
Nicodemus Minde, Marie-Aude Fouéré (17 mars 2026). Sehemu ya #3 Miili ya kigeni, vijana waliopotoshwa: Hotuba ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan, 3 Novemba 2025. Mambo ! Consulté le 12 juin 2026 à l’adresse https://doi.org/10.58079/15vzz
