Ressources numériques en sciences humaines et sociales OpenEdition Nos plateformes OpenEdition Books OpenEdition Journals Hypothèses Calenda Bibliothèques OpenEdition Freemium Suivez-nous

Sehemu ya #4. Jinsi vyombo vya habari vya Kenya vilivyoripoti mwelekeo wa Tanzania katika ukandamizaji wa serikali kupitia vichwa vya habari vya gazeti la The Standard (29 Oktoba–10 Novemba 2025)

Marie-Aude FOUÉRÉ & Nicodemus MINDE, “Sehemu ya #4. Jinsi vyombo vya habari vya Kenya vilivyoripoti mwelekeo wa Tanzania katika ukandamizaji wa serikali kupitia vichwa vya habari vya gazeti la The Standard (29 Oktoba–10 Novemba 2025)” Mambo! no. 109, 2026

Kwa siku nane mfululizo, kuanzia siku ya kupiga kura (Jumatano 29 Oktoba 2025) hadi siku mbili baada ya sherehe rasmi ya kuapishwa kwa rais mpya wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kurasa za mbele za gazeti la kila wiki la Kenya The Standard zilifuatilia kwa karibu kile kilichoelezwa kuwa kushuka kwa hatua kwa hatua kuelekea ukandamizaji wa serikali katika kipindi hiki muhimu cha upigaji kura na siku za mwanzo baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania wa 2025. Kurasa hizo za mbele zilisimulia, siku baada ya siku, namna maandamano yaliyolipuka katika miji mikubwa ya Tanzania kuanzia alasiri ya siku ya uchaguzi yalivyokabiliwa na ukandamizaji mkali na ghasia za kikatili. Hatua kwa hatua The Standard ilijaribu kuripoti maandamano hayo pamoja na hatua zilizochukuliwa kuyadhibiti, hata wakati mtandao wa intaneti, mitandao ya kijamii na mawasiliano ya simu za kimataifa yalikatizwa (Minde, 2025).

Nchini Kenya, gazeti la The Standard ni miongoni mwa magazeti yanayosomwa sana, pamoja na The Daily Nation. Pia ni “mojawapo ya magazeti jasiri zaidi,” likisemekana “kuisumbua serikali ya Kenya” (Ogongo-Ongong’a & White, 2008, uk. 172). Waandishi wengi wa habari wa Kenya “huchukulia kwa uzito sana jukumu lao la ‘kuisimamia serikali’ wakifuatilia shughuli zote za serikali,” na wanahisi kwamba wajibu wao wa kijamii na kiraia ni “kufichua kinachoendelea nyuma ya pazia ya mamlaka” (Ibid., uk. 168). Katikati ya kuimarishwa kwa utawala wa kimabavu nchini Kenya chini ya utawala wa Rais Ruto, na takriban mwaka mmoja tu baada ya serikali kukandamiza maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen-Z na Millennial wa Kenya (ambao madai yao yalijikita zaidi katika dhuluma za kiuchumi), vyombo vya habari vya Kenya vilifuatilia kwa jicho kali na la uchambuzi hali ya uchaguzi nchini Tanzania..

Ufuatiliaji huu wa vyombo vya habari vya Kenya una umuhimu mkubwa zaidi kwa sababu nchini Tanzania vyombo vya habari vimedhibitiwa kwa kiwango kikubwa, na kujizuia kuchapisha au kuripoti (self-censorship), kama hatua ya tahadhari, imekuwa jambo la kawaida (Grösswiler, 1997; Mwainyekule, 2025). Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 (Media Services Act) inafanya kosa la jinai kwa kashfa (defamation) na inampa serikali mamlaka ya kusimamisha gazeti, jambo ambalo hutokea mara kwa mara pale ambapo mwanasiasa wa ngazi ya juu wa chama tawala (CCM – Chama Cha Mapinduzi), au hata utawala wa muda mrefu wa zaidi ya miaka hamsini wa CCM, unapokosolewa (Matumaini, 2011; Rioba 2008; Powell 2017).

Katika kipindi cha angalau miaka 15 iliyopita kumekuwepo mifano mingi ya magazeti yaliyosimamishwa pamoja na kukamatwa, kunyanyaswa, kutoweka au hata kuuawa kwa waandishi wa habari. Kama ilivyobainishwa hivi karibuni na Reporters Without Borders (2021), nchini Tanzania waandishi wa habari wanapaswa “kuongozwa na uzalendo kwa taifa,” na utawala uliopo hauwezi kuvumilia waandishi wanaojaribu “kulichafua jina la nchi.”

Kurasa za mbele za The Standard zilizoripoti mabadiliko ya ukandamizaji katika mzunguko wa mwisho wa uchaguzi wa Tanzania ni za kuvutia zaidi kwa sababu zilisambazwa kwa wingi katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii (kama vile Facebook, Instagram na X) na mashirika ya haki za binadamu ya Kenya. Hii ilitokana na vichwa vya habari vyake vyenye ukosoaji mkali pamoja na picha zenye athari kubwa ya kihisia. Kwa njia hiyo, maudhui hayo pia yalisambaa ndani ya Tanzania na kuchochea uhamasishaji dhidi ya kuongezeka kwa utawala wa kiimla wa chama-dola tangu Samia Suluhu Hassan aingie madarakani kufuatia kifo cha Rais John Magufuli mnamo Machi 2021, wakati huo akiwa Makamu wa Rais. Mafanikio ya vichwa vya habari vya The Standard pia yanatokana, kwa upana zaidi, na utamaduni wa vyombo vya habari vya magazeti katika Afrika Mashariki pamoja na desturi hai ya kusoma magazeti ambayo huchochea mijadala mikali kuhusu maisha ya kisiasa—utamaduni ulioanza wakati wa ukoloni na kuimarika zaidi baada ya uhuru (Hunter, 2008; Frederiksen, 2011). Siku hizi vyombo vya habari vinapatikana kwa urahisi kwa kuwa kila gazeti lina tovuti yake na matoleo ya kidijitali yanapatikana mtandaoni. Hali hii inawezesha wasomaji kusambaza na kushiriki maudhui kwa upana zaidi kupitia mitandao ya kijamii.

Vichwa vya habari vya magazeti vinaathiri sana namna wasomaji wanavyofahamu yaliyomo ndani ya gazeti na jinsi wanavyotafsiri habari. Vinakuwa kama lenzi ya tafsiri ya habari (media framing) inayounda mtazamo wa msomaji hata kabla hajaisoma makala kamili. Kwa kawaida, vichwa vya habari hutambulisha tatizo, huonyesha nani anawajibika, na mara nyingi hutoa hukumu za kimaadili kupitia lugha na picha zinazotumiwa. Vyombo vya habari hutumia aina mbalimbali za fremu za uwasilishaji wa habari, kama vile fremu ya matukio (episodic frame) inayolenga tukio mahususi au la kusisimua ili mara nyingi kuonyesha uwajibikaji wa mtu binafsi badala ya sababu za kimfumo (Iyengar, 1991; Boukes, 2022).

Lengo la uchambuzi huu wa kina wa kurasa za mbele za The Standard ni kutoa maelezo ya siku kwa siku ya jinsi matukio ya ukandamizaji nchini Tanzania yalivyowasilishwa na kuelezewa, kwa kuzingatia mtazamo mpana wa mwaka huu wa uchaguzi, maandamano yaliyoambatana nao na yasiowaho kutokea tangu nchi ipate uhuru, na mwelekeo wa ukandamizaji mkali sana uliofanyika na serikali. Kama tutakavyoona, ni muhimu kujumuisha katika uchambuzi wetu jalada la mwisho la The Standard, lililochapishwa mnamo Novemba 10, yaani, siku tano baada ya ufuatiliaji wa wiki moja wa kupiga kura na wa siku chache baada yake, na wakati The Standard lilipoanza kuripoti kuhusu kesi ya wanaharakati wawili wa kutoka Kenya, Bob Njagi na Nicholas Oyoo, ambao walikuwa wamekamatwa na kufungwa na kuteswa katika magereza ya Uganda. Ukurasa huu wa mbele wa tarehe 10 Novemba unaweka matukio ya ukandamizaji Tanzania katika muktadha mpana wa ukandamizaji unaoendelea wa kiimla unaoathiri Afrika Mashariki, hasa majirani wawili wa Tanzania, Uganda na Kenya, katika kile kinachoitwa uundaji wa fremu ya kimuktadha (thematic framing) (Iyengar, 1991).

Ifuatayo ni orodha kamili ya tarehe na vichwa vya habari vya kurasa za mbele za The Standard vilivyochaguliwa na kujadiliwa katika uchambuzi huu. Majalada halisi, pamoja na vichwa vya habari vilivyonukuliwa na aya za mwanzo, vinawasilishwa moja baada ya nyingine sambamba na maelezo yetu kwa karibu.

  1. Jumatano 29 Oktoba – “Samia vs Suluhu”
  2. Alhamisi 30 Oktoba – “Defying Suluhu”
  3. Ijumaa 31 Oktoba – “Darkness in Dar”
  4. Jumamosi 1 Novemba – “Suluhu goes mute”
  5. Jumapili 2 Novemba – “Africa’s sham polls”
  6. Jumatatu 3 Novemba – “Tanzania massacre”
  7. Jumanne 4 Novemba – “A bloody crown”
  8. Jumatano 5 Novemba – “Suluhu’s vendetta”
  9. Jumatatu 10 Novemba – “Trinity of terror”

1. Jumatano 29 Oktoba. “Samia vs Suluhu” [Samia dhidi ya Suluhu]

Hakuna sauti. Upinzani umeondoloewa katika uchaguzi wa Tanzania, na kuugeuza kuwa mashindano ya upande mmoja (one-horse race). Maadili ya kidemokrasia ambayo Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuyasimamia sasa yanaonekana kuzikwa chini ya udhibiti mkali wa utawala wa kiimla. Wakati Watanzania wanaelekea kupiga kura leo, katika miji ya Arusha, Dar es Salaam na Moshi kumejaa hofu na wasiwasi—taifa linalopiga kura chini ya kivuli cha hofu, ukimya na hatima isiyoweza kuepukika.

Kichwa cha habari cha ukurasa huu wa mbele, “Samia dhidi ya Suluhu,” kinachochea dhana ya kuwa rais wa Tanzania mwenye nyuso mbili, kama hadithi ya Dr. Jekyll na Mr. Hyde. “Samia” ni jina lake la kwanza, linalobeba hisia ya ukaribu na urafiki. Pia ni “Mama Samia,” jina alilochagua kuitwa kwa upendo mwaka 2021 alipomrithi John Magufuli kama rais, huku akisisitiza sifa zake za kike : upendo, huruma na msamaha…(Munisi & Skerdal, 2025). Suluhu ni jina lake la pili na la katikati, ambalo hutumika mara chache lakini lina uzito wa kiishara kwa sababu linamaanisha ‘maridhiano’ au ‘suluhisho’. Tangu alipoingia madarakani mwaka 2021, vyombo vya habari vya Kenya vimekuwa vikimtaja mara nyingi kwa jina hili, ishara ya urithi wa pamoja wa Kiswahili kati ya mataifa haya mawili. Uamuzi wa kumwonyesha katika picha ya jalada akiwa amevaa sare ya kijeshi—ikizingatiwa kuwa rais wa Tanzania pia ni Amiri Jeshi Mkuu—unamrejelea kama mwanamke wa vita, mkakati na asiye na huruma. Pia unaashiria utawala wa kimabavu uliopo nchini Tanzania. Aya ya utangulizi inatukumbusha kwamba, kabla tu ya uchaguzi, mchezo ulikuwa tayari umechezwa, kwa kuwa wapinzani wakuu wa Samia Suluhu Hassan—hasa Tundu Lissu—walikuwa wamezuiwa kugombea kwa mbinu mbalimbali za kisiasa. Aya hiyo inamalizia kwa maelezo ya hali ya mvutano mkali kabla ya siku ya kupiga kura, ikionyesha mchanganyiko wa hofu na kukata tamaa. Maneno “one-horse race” na “inevitability” yanasisitiza wazo hilo: ikiwa Samia Suluhu Hassan ndiye mgombea pekee, basi ushindi wake unaonekana kuwa tayari umeamuliwa. Neno “autocratic” (utawala wa kimabavu) linaonekana tayari katika jalada hili la kwanza kuelezea kuimarika kwa udhibiti wa utawala juu ya jamii tangu alipoingia madarakani. Marejeleo kwa Julius Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania na baba wa taifa, ni sehemu ya simulizi kuu ya kitaifa ya Tanzania (Fouéré, 2015). Lakini pia Nyerere ni kiongozi anayeheshimiwa sana nchini Kenya. Hivyo The Standard inaweza kurejea maadili ya kidemokrasia yaliyochochea harakati za uhuru Afrika Mashariki, na kusisitiza kuwa utawala wa kiimla si tu ukiukaji wa haki za binadamu bali pia usaliti wa maadili ya msingi ya taifa.

2. Alhamisi 30 Oktoba. “Defying Suluhu” [Kumpinga Suluhu]

“Nguvu ya Wananchi: Tanzania iko katika hali ya taharuki huku maandamano ya vurugu yakizuka katika miji mikuu, mamia ya vijana wenye hasira wakipuuza amri za polisi na kulaani kile wanachokiita uchaguzi wa udanganyifu. Rais Samia Suluhu Hassan anakaribia kushinda kwa urahisi baada ya kuwaondoa viongozi wa upinzani katika uchaguzi na kuimarisha udhibiti wake wa madaraka. Barabara zinawaka moto, intaneti imezuiwa, na usafiri wa umma umesimama kabisa katika hali isiyokuwa ya  kawaida ya kupinga.”

“Nguvu ya Wananchi” ni kaulimbiu ya CHADEMA (Chama cha Demokrasia na Maendeleo), chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania chenye msingi imara na wafuasi wengi kote nchini (Paget, 2019). Tundu Lissu, kiongozi jasiri na asiyeyumba kimsimamo (Minde, 2024), amekuwa mwenyekiti tangu Januari 2025, lakini alikamatwa mwezi Aprili 2025 na kesi yake ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo imekuwa ikiendelea.[1] Kama ilivyokuwa siku iliyotangulia, aya kuu inarejelea hili kwa utulivu, pamoja na kukamatwa kwa wapinzani wengine. Aidha, inaonyesha tena kuharakishwa kwa hatua za udhibiti wa kisiasa na utawala uliopo madarakani tangu Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani mwaka 2021. Katika muktadha huo, kichwa cha habari cha ukurasa wa mbele kinatumia tena jina Suluhu badala ya Samia: Samia hayupo tena, kilichobaki ni upande wake wa giza, Mr. Hyde wake. Maelezo ya hali ilivyo nchini yanaakisi mabadiliko ya haraka yaliyotokea: tunatoka katika hali ya kusubiri kwa tahadhari ya siku iliyotangulia hadi kufikia hali ya taifa kuwa “kwenye taharuki.” Kwa hakika, kuanzia alasiri ya Siku ya Uchaguzi, idadi kubwa ya vijana walijitokeza mitaani katika miji mikuu ya Tanzania kupinga kile walichodai kuwa uchaguzi wa udanganyifu, kupinga kuongezeka kwa utawala wa kiimla, na kudai kuondoka kwa CCM (Chama Cha Mapinduzi), chama tawala ambacho kimetawala siasa za taifa tangu uhuru (Makulilo, 2008; Minde, 2021). Ukurasa wa mbele, unaotoa muhtasari mpana wa hali ilivyokuwa (uharibifu na uchomaji moto, kusimama kwa usafiri, kukatizwa kwa Intaneti), unahitimisha kwa wazo kuu la “onyesho la ukaidi” kwa mamlaka ya kisiasa, na kwa rais hasa, likiongozwa na vijana wenye hasira, jambo linaloakisi kichwa cha habari, “Defying Suluhu” [Kumpinga Suluhu]. Kwa mujibu wa gazeti la Standard, vijana hawa wanaonekana kuwakilisha wananchi wa Tanzania kwa ujumla (Nguvu ya Wananchi) na/au pengine kuwa wafuasi wa CHADEMA, au kwa upana zaidi, wafuasi wa upinzani. Picha ya jalada inaonyesha vijana hao wakiwa na amani lakini wakidhibitiwa na maafisa wa polisi wenye silaha nzito pamoja na magari yao makubwa ya 4×4.

3. Ijumaa 31 Oktoba. “Darkness in Dar” [Dar katika giza]

Ukaidi. Tanzania imeingia katika machafuko makali ya kisiasa katika huku wananchi wenye hasira wakimiminika mitaani kukataa kile wanachokiita uchaguzi ulioibiwa. Mahali alipo Rais Samia Suluhu bado hakujulikani wakati nchi ikiwa katikati ya amri ya kutotoka nje, kukatwa kwa intaneti na vifo vinavyoendelea kuongezeka. Mipaka ikiwa katika hali ya tahadhari na jeshi likiwaonya polisi wasiwapige risasi waandamanaji, dunia inatazama jinsi taifa lililowahi kusifiwa kwa utulivu wake linavyozama katika machafuko.

Ukurasa huu wa mbele unaendeleza wazo lililoanagziwa siku iliyotangulia kuhusu vijana wanaodhaniwa kuwa na msimamo wakpinga mamlaka ya chama tawala na pia kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika hivi karibuni. Tunafahamu kwamba, siku mbili baada ya kura kupigwa na kuanza kwa ukandamizaji, rais mteule haonekani. Uso wake, uliokuzwa kwenye ukurusa wa mbele, unaonyesha sura ya kutokuwa na wasiwasi wala kujali. Aya ya mwanzo inakumbusha hali ilivyo nchini, inayofanana na ya siku iliyotangulia (kama inavyoonyeshwa na picha mbili ndogo zaidi zilizopo kwenye ukurasa wa mbele), pamoja na amri ya kutotoka nje usiku. Pia inaonyesha kwamba ukatili uliotumika kukandamiza maandamano umesababisha vifo na sasa unaenea hadi katika mpaka wa kaskazini wa nchi ya Kenya. Aidha, inaongeza kipengele kipya: mgawanyiko ndani ya vikosi vya usalama kati ya, kwa upande mmoja, polisi, ambao wanasemekana kuongoza operesheni ya ukandamizaji, na kwa upande mwingine jeshi, ambalo linaonekana kujaribu kutuliza hali. Kichwa cha habari “Dar in Darkness” [Dar katika giza] kinaweza kusomwa kwa maana ya moja kwa moja (kama inavyoonekana kwenye picha ya ukurasa wa mbele inayoonyesha jiji wakati wa usiku, likiwa limewaka kwa jengo linalowaka moto); lakini pia kwa maana ya kifumbo, kikiwa kinarejelea ukandamizaji mkali unaoendelea. Aya ya mwanzo pia inasisitiza jinsi ukandamizaji huo wenye umwagaji damu ulivyoshangaza watu wengi duniani. Aidha, inaangazia upekee wa tukio hili laukandamizaji, ambalo si la kawaida katika nchi inayojivunia historia ya “amani na utulivu” na ambako tangu uhuruchama-dola kimeendesha aina ya utawala wa kiimla ambao watu hawapingi, badala ya udhibiti wa kijamii wenye vurugu na mauaji (Maingraud-Martinaud & Fouéré, 2015).

4. Jumamosi 1 Novemba. “Suluhu goes mute” [Suluhu kimya]

Machafuko.” Rais Samia Suluhu aendela kuwa kimya huku umwagaji damu ukizidi. Ripoti zinazokinzana zinaashiria kuwa hadi Watanzania 700 huenda wameuawa huku maandamano dhidi ya uchaguzi wenye utata yakienea kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Arusha. Wakati njia za mawasiliano bado zimekatwa, hofu na hasira vimeikumba nchi nzima huku matokeo rasmi yakisubiriwa wakati wowote sasa. Viongozi wa kikanda (Afrika Mashariki) wanaendelea kubaki kimya kwa njia inayoenekana wazi, huku dunia ikitazama Tanzania ikizama katika machafuko.

Kama ilivyo tangu Oktoba 29, ukurasa wa mbele unaendelea kumtaja rais mteule kama ‘Suluhu’, jina ambalo sasa limechukua maana ya upande wake wa giza. Siku moja imepita lakini mshindi (pamoja na viongozi wengine wa kisiasa) bado hajapatikana, huku “machafuko” yakitawala, neno linaloakisi “vurugu” iliyotimiwa siku iliyotangulia na kurudiwa tena mwishoni mwa aya ya mwanzo wa habari. Serikali inatafuta mbinu ya kuzuia mtiririko wa habari kuhusu hali inayoendelea (mawasiliano bado yamekatwa) huku idadi ya vifo ikiendelea kuongezeka. Picha ya ukurasa wa mbele, inayoonyesha afisa wa polisi mwenye hasira akimkamata mwananchi mmoja kwa nguvu kubwa, inavutia zaidi kwa kuwa wahusika hao wawili wanaonekana kama wanatazamana kwa ukali. Ukurasa wa mbele unataja idadi ya vifo 700 lakini pia unasisitiza kutokuwa na uhakika na takwimu hizo. Kipengele kingine kipya kinachojitokeza katika aya huu kinahusu matokeo ya uchaguzi: siku tatu zimepita, kura zinaendelea kuhesabiwa, na nchi inasubiri matokeo—huku ikijua, kama ilivyoonyeshwa kwenye ukurasa wa mbele wa tarehe 29 Oktoba, kwamba ushindi wa Samia Suluhu Hassan ni wa hakika. Sentensi ya mwisho inaelezea mshangao na hali ya kutoweza kufanya chochote kwa jumuiya ya kimataifa mbele ya wimbi la vurugu lililoiubuka.

5. Jumpili 2 Novemba. “Africa’s sham polls” [Uchaguzi bandia wa Afrika]

Demokrasia majaribuni. Uchaguzi wa urais nchini Tanzania umetoa ushindi wa kushangaza wa asilimia 98 kwa Rais Samia Suluhu Hassan – takwimu inayoenekana kuwa sio ya ukweli na kuchekesha. Huku viongozi wa upinzani wakiwa gerezani, kiwango cha ushiriki kwa wapiga kura kikionekana kupindishwa, na taifa likiwa limezamishwa katika giza la kukatiwa mtandao wa intaneti, kilichotokea kilifanana zaidi na kutawazwa kwa kiongozi kuliko uchaguzi wa kidemokrasia. Ili kuonyesha kile kilichiitwa ‘ufanisi’, maafisa wa uchaguzi walihesabu kura milioni 33 ndani ya siku mbili. Hata hivyo, swali sasa ni nini kinafuata kwa Suluhu. Huenda amepata madaraka, lakini uhalali wa utawala wake umepungua. Kurejesha imani ya wananchi nyumbani na kuimarisha uaminifu kimataifa kutahitaji zaidi ya matamko ya ushindi yaliyopangwa na kuratibiwa kisiasa.

Matokeo ya uchaguzi yalitangazwa siku moja kabla ya ukurasa huu wa mbele wa The Standard, na kwa mujibu wa gazeti hilo yalikuwa ya kushangaza sana na wakati huo huo ya kuchekesha: rais alichaguliwa kwa asilimia 98 ya kura. Kiwango cha ushiriki cha asilimia 87 kinaonekana pia kinachukuliwa kuwa cha kutia shaka. Idadi ya kura zilizopigwa (milioni 33) pamoja na muda mfupi sana uliotolewa kuzihesabu kwa mkono (ukizingatia kwamba Tanzania bado inatumia kura za karatasi zilizowekwa katika masanduku za plastiki) zimeangaziwa ili kusisitiza hali ya kutokuwa na mantiki ya matokeo hayo. Hii ndiyo sababu aya ya mwanzo ya habari inazungumzia “kutawazwa” badala ya uchaguzi (Collord, 2025), na kumfanya Samia Suluhu Hassan aonekane kama mfalme ambaye amefanya tu upya mamlaka yake, badala ya kuwa mgombea aliyechaguliwa kidemokrasia, yaani, kuwa chaguo la watu. Kichwa cha habari kinawakumbusha wasomaji kwamba taarifa kuhusu hali halisi nchini bado zinazuiwa na utawala na kwamba upinzani unakatazwa kujieleza. Wakati huo huo, idadi ya vifo inaongezeka hadi 800. Hata hivyo, jalada hili linabadilisha mtazamo wa lugha: sasa linaukosoa uchaguzi hio moja kwa moja kwa sauti yake yenyewe (katika makala zilizotangulia, ilionyesha tu kwamba vijana walioandammana walikuwa wanaukosoa). Pia inabainisha kwamba, katika hali ambayo rais mpya hana halali wa kisiasa, kwa kuwa hakuweza kuchaguliwa kwa kwa njia inayoonekana kuwa halali na anakabiliwa na changamoto ya kujijengea uhalali wake wa kisiasa nchini Tanzania na katika ngazi ya kimataifa. Hili ni kazi ngumu sana ambayo haiwezi kupunguzwa kuwa mapambano ya kisiasa au maonyesho ya juu juu, linasisitiza gazeti la The Standard kwa dhihaka.

6. Jumatatu 3 Novemba. “Tanzania massacre” [Mauaji ya kimbari Tanzania]

Nguvu isiyo na kipimo. Kama Mwalimu Julius Nyerere angeweza kurudi katika taifa alilolijenga juu ya misingi ya umoja wa Afrika, bila shaka angeshutuka sana. Wakati rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania alipopigania kuhakikisha anapata mamlaka yake mwenyewe, damu ilimwagika kote nchini. Wakiwa wametengwa na dunia wakati wa na baada ya upigaji kura, Watanzania walipitia kile ambacho makundi ya haki za binadamu sasa yanakitaja kama umwagaji mkubwa wa damu, uliokuwa umefichwa nyuma ya kuzima rasmi kwa mawasiliano, lakini ukawekwa wazi kupitia taarifa zilizoshirikiwa na wenzao wa Kenya.

Kichwa hiki cha ukurasa wa mbele kinarudia baadhi ya vipengele vilivyoripotiwa katika siku zilizotangulia kuhusu ukandamizaji mkali unaoendelea. Hata hivyo, matumizi ya neno “mauaji ya halaiki” (massacre) katika kichwa cha habari—linaloendana na neno “bloodbath” lililotumiwa na wanaharakati wa haki za binadamu kuelezea hali hiyo—linadokeza kwamba kiwango cha vurugu na idadi ya waathiriwa ni kubwa kiasi kwamba haviwezi tena kukubalika au kuelezwa kama matukio ya pekee au vitisho vya kawaida. Picha ya jalada inaonyesha picha za kushtua za miili iliyoharibiwa, katika rangi nyeusi na nyeupe, zinazoonyesha ukatili wa hali ilivyo. Taswira ya baba wa taifa, Julius Nyerere, inatajwa tena ili kuelezea kile kinachoonekana kama usaliti wa kimaadili unaotokea. Hii hairejelei tu “maadili ya kidemokrasia,” kama ilivyokuwa katika jalada la kwanza la mfululizo huu wa The Standard tarehe 29 Oktoba, bali pia kwa upana zaidi maadili ya “umoja wa Afrika.” Katika muktadha huu, dhana hiyo inaonekana kumaanisha zaidi umoja wa ndani ambao kila taifa linapaswa kuujenga na kuudumisha. Aya ya mwanzo ya habari pia ni ya kuvutia kwa sababu inapendekeza kuwepo kwa mtandao madhubuti wa mawasiliano na mshikamano kati ya wanaharakati, ambapo mashirika ya Kitanzania yanawasilisha taarifa wanazopata moja kwa moja kutoka uwanjani kwa wenzao wa Kenya ili waweze kuzisambaza kwa upana zaidi. Katika hali hii, tuhuma zinaongezeka kwamba utawala uliopo madarakani ulizima kwa makusudi mtandao wa intaneti ili kuweza kutekeleza mauaji bila kuadhibiwa.

7. Jumanne 4 Novemba. “A bloody crown” [Taji la damu]

Siku ya Madikteta. Ukimuondoa Hakainde Hichilema wa Zambia, ambaye kukwea kwake kutoka jela chini ya uongozi wa Edgar Lungu kunafanana na hali ya Tundu Lissu wa Tanzania, viongozi wengi waliokusanyika Dodoma kwa ajili ya kuapishwa kwa Rais Samia Suluhu walibeba doa linalofanana. Miongoni mwao alikuwa Naibu Rais wa Kenya, Kithure Kindiki, ambaye taswira yake ya kisiasa imeathiriwa na maandamano ya kizazi Z (Gen Z) ya mwaka jana yaliyosababisha vifo vya watu wengi. Walisisimama pamoja, walionekana kama ushirika wa mamlaka uliobobea katika kunyamazisha upinzani, kulinda tawala zao dhidi ya uchunguzi wa umma na kuhakikisha ushindi kupitia mazingira ya chaguzi zenye utata.

Sherehe ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan kama Rais wa Tanzania ilifanyika siku moja kabla ya ukurasa huu wa mbele. Picha ya ukurusa huu inamuonyesha akiapishwa, huku moto ukiwaka nyuma yake na, kwa mara nyingine tena, picha nyeusi na nyeupe za kutisha zinazoonyesha athari za vurugu kwa waathiriwa. Ilikuwa sherehe ya kuapishwa iliyofanyika kwa haraka sana, takribani siku mbili tu baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa, ambapo rais alijitokeza na kuzungumza hadharani kwa mara ya kwanza tangu ukandamizaji kuanza (lakini The Standard haitaji kwamba wakati huohuo kulikuwa na uwezekano wa hatari kwa serikali kupinduliwa).[2] Kichwa cha habari, “Taji la damu,”(A Bloody Crown) kinaunganisha wazo lililotolewa awali la kutawazwa kwa kifalme, kinyume na misingi ya demokrasia iliyowekwa katika Katiba ya Tanzania, pamoja na ukandamizaji mkali unaosababisha vifo na unaokiuka haki za binadamu na viwango vya maadili. Hii ndiyo sababu kiongozi huyo anamithilishwa kama “dikteta.” Aya ya mwanzo inaeleza kwamba waliohudhurua sherehe hiyo walikuwa has wakuu wa nchi au manaibu wao mabao wanahusishwa na mienendo ya kiimla kama Samia Suluhu Hassan na ambao pia wanadaiwa kuwa na “doa” la umwagaji damu (isipokuwa rais wa Zambia). Hii ni fursa kwa The Standard kumkosoa vikali Naibu Rais wa Kenya Kithure Kindiki, kwa kumkumbusha ukandamizaji uliosababisha vifo vya vijana wa Kenya waliokuwa wakiandamana katika maandamano ya Gen Z mwaka mmoja uliopita. Aidha, hoja hii inatumika kutoa tamko muhimu kuhusu uwepo wa ushirikiano usio rasmi kati ya viongozi wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki zenye utawala wa kiimla ambaoo wanawanyanyasa wapinzani (wa vyama na wananchi) na kudhoofisha demokrasia ili kuendelea kubaki madarakani kwa gharama yoyote ile. 

8. Jumatano 5 Novemba. “Suluhu’s vendetta” [Suluhu akilipiza kisasi]

Kisasi. Tanzania imeanzisha msako mkali dhidi ya wageni wanaotuhumiwa bila hatiakuwa wamechochea vurugu za baada ya uchaguzi, polisi na wanajeshi wamevamia hoteli, wameimarisha udhibiti wa mipaka na kuwakamata baadhi ya wananchi wa Afrika Mashariki bila sababu za msingi. Amri hiyo, iliyotolewa kutoka makao makuu ya polisi mwishoni mwa Jumatatu, imesababisha mshtuko mkubwa katika sekta ya utalii na kusababisha hofu miongoni mwa Wakenya wanaoishi nchini.

Je “Suluhu” anataka kulipiza “kisasi” kwa nini? Kwa mara ya kwanza katika wiki moja, tunaona msako mkali unawaathiri sana wageni, hasa Wakenya waishio Tanzania. Msako huu wa watu wasio na hatia lazima ueleweke kwa kurejelea hotuba ya kuapishwa kwa rais mteule, ambapo alidai kuwa wale waliohusika katika ghasia hizo walikuwa raia wa kigeni kwa kiasi kikubwa, huku Watanzania, walio watiifu kwa taifa lao, wasingeweza kufanya maandamano kama hayo.[3] Kwa njia hii, Samia Suluhu Hassan anajaribu kudumisha dhana potofu ya uhalali wake wa ndani kupitia matumizi ya kauli za kitaifa za kawaida kuhusu amani, utulivu, na uzalendo/utanzania. Kwa sasa, vyombo vya usalama vinaonekana kuungana kikamilifu katika kufanya ukandamizaji, na mgawanyiko wa ndani ulioashiriwa na gazeti la The Standard kwenye ukurasa wake wa mbele wa tarehe 31 Oktoba haionekani tena kutumika tangu kuapishwa kwa rais – au linapokuja suala la kukandamiza watu wasio Watanzania. Picha ya Samia Suluhu Hassan akiwa amevaa sare ya kijeshi, ile ile iliyotumika katika toleo la Oktoba 29, inaonekana kwenye ukurasa wa mbele: Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama anaonekana kuwa amerejesha udhibiti wa hali ya usalama nchini.

9. Jumatano 10 Novemba. “Trinity of terror” [Utatu wa hofu]

Ukandamizaji unaongezeka. Wakati Yoweri Museveni wa Uganda alipokiri kwamba Wakenya wawili waliteswa wakiwa chini ya ulinzi wa mamlaka ya nchi yake, bila kukusudia alichochea zaidi wimbi la ukandamizaji linaloenea kote Afrika Mashariki. Aliyewahi kuonekana kama kama mzee wa busara wa ukanda huu, Museveni sasa anazungumza wakati dunia bado inashtushwa na umwagaji damu ulioambatana na uchaguzi wa 29 Oktoba wa Tanzania uliompa Rais Suluhu ushindi wa jumla na kumjengea sifa mpya ya utawala wa kidhalimu. Nchini Kenya, udongo bado haujakauka vizuri juu ya makaburi ya vijana waliouawa, huku wengine bado wakiwa wamepotea. Afrika Mashariki inaanza kufanana na Ulaya ya miaka ya 1930, iliyokuwa chi ya tawala za Adolf Hitler, Benito Mussolini na Ion Antonescu.

Jalada hili la mwisho la The Standard tulilojumisha katika uteuzi wetu linatoka siku tano baada ya kuripoti kwa wiki nzima kuhusu ukandamizaji uliopo nchini Tanzania. Wakati huo huo, gazeti hilo lilikuwa limenza kuripoti kuhusu hali ya wanaharakati wawili wa Kenya, Bob Njagi na Nicholas Oyoo, ambao walikamatwa na kuteswa katika magereza ya Uganda – tuhuma ambazo Rais Yoweri Museveni alikuwa amezikanusha kwa siku kadhaa. Ukurasa huu wa mbele wa tarehe 10 Novemba unatoa muktadha mpana zaidi kwa matukio ya ukandamizaji nchini Tanzania, ukiyahusisha na wimbi pana la ukandamizaji wa kiimla unaoendelea Afrika Mashariki, hasa nchini Uganda na Kenya. Ili kuwasilisha wazo hili, jalada linaweka picha za bega kwa bega za Samia Suluhu Hassan, Yoweri Museveni, na William Ruto, wakivaa sare zao za kijeshi za Amiri Jeshi Mkuu, kando kwa kando. Aya ya mwanzo ya habari inakumbusha ukandamizaji wa kikatili nchini Tanzania na inataja suala ambalo lilianza kupata uzito katika siku zilizofuata na mabalo bado linaendelea hadi sasa – kutoweka kwa miili na waathiriwa na juhudi za familia za kutafuta ndugu zao waliokufa. Utangulizi unaishia kwa kulinganisha na serikali za kiimla za Ulaya za miaka ya 1930, ikifananisha viongozi wa sasa wa nchi za Kenya, Uganda, na Tanzania na majina mabaya zaidi ya fedhea ya kimaadili ambayo historia imewahi kukumbuka.

Mfululizo huu wa makala ya Mambo! unajikita katika kuelezea mwaka wa uchaguzi wa 2025 nchini Tanzania. Unatoa maelezo ya kipekee wa usomaji wa kina na ukaribu wa vielelezo vya matukio ya kisiasa ya mwaka huu wa uchaguzi, uliokua na matukio mengi na uliotawaliwa na muendelezo wa ukandamizaji wa serikali. Katika kila sehemu cha mfululizo huu, tukio lililochaguliwa linazalishwa tena katika asili yake na kutafsiriwa panapohitajika, likiwekwa katika muktadha kwa uangalifu na kufafanuliwa au kupewa maelezo ya karibu kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa kuelewa kwa kina sehemu lilipotokea pamoja na maana na umuhimu wake. Matukio haya ni vyanzo ama nyaraka ya maana kwa ajili ya kuchambua muendelezo wa utawala wa kimabavu na ukandamizaji wa wazi uliofanywa na serikali ya Tanzania katika kipindi hiki cha uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2025.

Marejeo

Boukes, M. (2022). Episodic and thematic framing effects on the attribution of responsibility: The effects of personalized and contextualized news on perceptions of individual and political responsibility for causing the economic crisis. The International Journal of Press/Politics, 27(2), 374–395.

Collord, M. (2025, November 4). After the coronation. Africa is a Country. https://africasacountry.com/2025/11/after-the-coronation

Fouéré, M.-A. 2015. ‘Julius Nyerere’: The Man, the Word, and the Order of Discourse. In M.-A. Fouéré, Remembering Nyerere in Tanzania: History, Memory, Legacy (p.3–32). Mkuki na Nyota/Africae. https://books.openedition.org/africae/703

Iyengar, S. (1991). Is anyone responsible? How television frames political issues. University of Chicago Press.

Maingraud-Martinaud, C. & Fouéré, M.-A. (2015). Une hégémonie compétitive contre vents et marée: Les élections générales de 2015 en Tanzanie. Politique africaine 140(4), 145-163. https://doi.org/10.3917/polaf.140.0145

Makulilo, A. (2008). Tanzania: A de facto one party state? VDM Verlag.

Minde, N. (2025, November 5). Denied fair elections, Tanzanians make their mark through protests. ISS Today. https://issafrica.org/iss-today/denied-fair-elections-tanzanians-make-their-mark-through-protests.

Minde, N. (2021). The Endurance of One-Party Dominance: The Chama Cha Mapinduzi (CCM) Party and the Challenge of Democratizing the Tanganyika-Zanzibar Union. PhD Diss., United States International University-Africa

Mwainyekule, L. (2025, September 27). Tanzania’s social media clampdown and the elections — what’s at risk. The Conversation. https://theconversation.com/tanzanias-social-media-clampdown-and-the-elections-whats-at-risk-265215

Paget, D. (2019). The Authoritarian Origins of Well-organized Opposition Parties: The Rise of Chadema in Tanzania. African Affairs, 118(473): 692-711. https://discovery.ucl.ac.uk/id/eprint/10079040/3/Paget_The%20authoritarian%20origins%20of%20well-organized%20opposition%20parties.%20The%20rise%20of%20Chadema%20in%20Tanzania_AAM.pdf  


Maelezo

[1] Kwa maelezo zaidi kuhusu Tundu Lissu, tazama sehemu ya 1 ya mfululizo huu.

[2] Kwa maelezo zaidi, tazama vipindi vya 2 na 3 vya mfululizo huu, vinavyomlenga Samia Suluhu Hassan.

[3] Tazama uchambuzi wa hotuba yake ya ufunguzi katika kipindi cha 3 cha mfululizo huu, hasa sehemu ya kuegenisha upinzani.

 


OpenEdition vous propose de citer ce billet de la manière suivante :
Marie-Aude Fouéré, Nicodemus Minde (24 mars 2026). Sehemu ya #4. Jinsi vyombo vya habari vya Kenya vilivyoripoti mwelekeo wa Tanzania katika ukandamizaji wa serikali kupitia vichwa vya habari vya gazeti la The Standard (29 Oktoba–10 Novemba 2025). Mambo ! Consulté le 16 avril 2026 à l’adresse https://doi.org/10.58079/15xni


Vous aimerez aussi...

Laisser un commentaire

Votre adresse e-mail ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.