Ressources numériques en sciences humaines et sociales OpenEdition Nos plateformes OpenEdition Books OpenEdition Journals Hypothèses Calenda Bibliothèques OpenEdition Freemium Suivez-nous

Sehemu ya #5. ‘Kura ni alama ya maendeleo’: Kuahidi maendeleo Zanzibar kupitia kampeni zilizotawaliwa na mabango ya kisiasa

Marie-Aude FOUÉRÉ & Nicodemus MINDE, “Sehemu ya #5. ‘Kura ni alama ya maendeleo’: Kuahidi maendeleo Zanzibar kupitia kampeni zilizotawaliwa na mabango ya kisiasa” Mambo! no. 110, 2026

Katika uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2025, maendeleo haikuashiria tu ‘maendeleo’—yalitumika kama teknolojia ya kisiasa (political technology) ambayo kupitia kwayo CCM (Chama cha Mapinduzi) ilijaribu kugeuza miundombinu kuwa uhalali wa kisiasa na kupiga kura kuwa kitendo cha utii uaminifu badala ya chaguo la wazi. Kama ilivyo kwa dhana yoyote, na hasa kwa dhana ambayo, kote Tanzania (ikiwemo Zanzibar), inabeba uzito wa historia ya ukoloni na ya baada ya ukoloni, maendeleo yana maana nyingi na zinazotegemea muktadha.[1] Kama anavyohoji Koponen (2018), “ni katika utata huu ndipo dhana hii hupata nguvu yake. Ingawa kila mtu anaweza kukubaliana na umuhimu wake, mambo mengi yanaweza kujumuishwa chini ya mwavuli wake”. Hivyo basi, maendeleo yalimaanisha nini kwa CCM katika mwaka wa uchaguzi wa 2025?[2] Au, kwa usahihi zaidi, CCM ilijaribuje kuwashawishi wapiga kura wa Tanzania kuhusu maana ya maendeleo, na pia kuwafanya wakubali wazo kwamba aina hii maalum ya maendeleo (badala ya nyingine yoyote) ndiyo iliyokuwa bora kwao—jambo ambalo lingewasukuma kupiga kura kwa CCM na wagombea wake? Kwa ujumla zaidi, maendeleo yana nafasi gani katika jitihada endelevu za CCM kudumisha kuhodhi utawala wa kisiasa Tanzania, na hasa Zanzibar?

Katika sehemu hii ya tano na ya mwisho ya mfululizo huu kuhusu uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025 tunaangazia maendeleo kama teknolojia ya kisiasa kupitia usomaji wa karibu (close reading) wa bango moja la kampeni la CCM huko Zanzibar.[3] Mabango ya kampeni na matangazo makubwa (billboards), ya ukubwa mbalimbali, ambayo yalijaza maeneo mbalimbali ya umma kote Zanzibar mwaka 2025, ni vitu halisi vya kisiasa vinavyoshikika (material objects) vinavyofaa sana katika kuchunguza muingiliano tata kati ya ujumbe wa kisiasa, diskosi, uhalisia na taswira vinavyounda dhana na lugha kuu ya maendeleo wakati wa kampeni za uchaguzi, kwa lengo la kuipa maana moja na ya kuvutia. Mabango haya ya kampeni yanakuza na kuakisi maendeleo kwa kuyapa sura halisi na inayoweza kueleweka ambayo kila mtu anapaswa kuielewa: yanakuonyesha hasa miundombinu kama barabara, bandari na viwanja vya ndege, hospitali na shule, na mara chache vituo vikubwa vya ununuzi. Kupitia kauli mbiu wanazotumia, ikiwemo ya “Kura ni alama ya maendeleo”, mabango pia yanatoa sauti kwa wajibu wa kiraia na kauli ya kimaadili. Hata hivyo, je, maendeleo, kama yanavyotangazwa na CCM, yanaendana na maono na matarajio ya wananchi wa leo? Na je, maelfu ya mabango yaliyotapakaa katika maeneo ya umma, kwa picha na kauli mbiu zake, yanaweza kufanikiwa kuwashawishi Wazanzibari kwamba, safari hii hatimaye, chama tawala kitatimiza ahadi ambazo hadi sasa zimekuwa zikitekelezwa kwa kiwango kidogo au kwa namna isiyoridhisha?

Mabango ya kampeni ya Zanzibar yenye kauli mbiu “Kura ni alama ya maendeleo”

Kilometa chache kutoka Uwanja wa Ndege wa Pemba, kwenye makutano ya barabara yanayopita katikati ya mtaa ambao watu wa kawaida wanaishi, bango kubwa la kampeni linatoa mkusanyiko wa taswira mbalimbali wa dhana ya maendeleo. Bango hilo linaonyesha jengo la rangi ya bluu ambayo haijakolea, ambalo usanifu wake unafuata mtindo wa majengo ya Kiarabu na Kiswahili ambao ni maarufu katika visiwa vya Zanzibar: hiyo ni Hospitali ya Wilaya ya Kinyasini, Mkoa wa Kaskazini Pemba, iliyofunguliwa rasmi mwezi wa Novemba wa mwaka 2023 wakati wa kipindi cha uongozi wa Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi. Picha ya Rais Mwinyi inaonekana mbele kwenye picha, kwenye kona ya kulia. Nyumba zilizoko jirani na bango hilo ni nyumba ndogo za makazi zilizojengwa kwa matofali ya saruji na kuezekwa kwa mabati, zikitenganishwa kwa njia nyembamba za vumbi. Vibaraza vidogo vilivyo mbele ya milango ya baraza—yaani mabenchi za zege yaliyounganishwa kwenye kuta za mbele—hutumika kwa kawaida na wakaazi kama maeneo ya kupumzika na kujumuika na majirani. Skuta, usafiri unaopendwa sana na watu wa tabaka la kati, ipo imeegeshwa chini ya bango hilo.

Bango la uchaguzi la ‘Kura ni alama ya maendeleo’ likionyesha hospitali mpya ya Kinyasini iliyofunguliwa Pemba mwishoni mwa mwaka 2023 © Picha na Ania Gruca, Oktoba 2025

Kwa kuwa picha haizungumzi yenyewe, bango hilo linajumuisha maandishi yaliyoandikwa ili kutoa muktadha wa tafsiri yake. Maneno haya, kwanza kabisa, ni kaulimbiu ‘Kura ni alama ya maendeleo’, ambayo inaimarisha wazo kwamba ni kuchaguliwa tena kwa CCM kuendelea kushika dola pekee —kupitia uhamasishaji wa kila mpiga kura siku ya uchaguzi, tarehe 29 Oktoba—kunaweza kuhakikisha utoaji wa huduma hizi za msingi za umma katika siku zijazo. Maneno haya yanaakisi kauli mbiu na misemo mingine kuu za ukuaji wa kiuchumi zilizotumiwa na CCM wakati wa kampeni ya 2025 kama vile, ‘Kazi na Utu’, ‘Kazi Iendelee’, na ‘Oktoba Tunatiki’, ambazo zinasisitiza upigaji kura kama kitendo cha kiutamaduni badala ya kuwa utaratibu wa kidemokrasia na wajibu wa kiraia unaowezesha kutolewa kwa maono tofauti ya kisiasa.[4] Kwenye bango, kaulimbiu hiyo pia inaambatana na wito wa kuichagua CCM na mgombea wake wa urais, Hussein Ali Mwinyi (‘Chagua CCM, Chagua Dkt. Hussein Ali Mwinyi’). Hakuna utata katika ujumbe huo. Maendeleo yaliyohadiwa hayawasilishwi kama matokeo ya utawala bora, bali yanawasilishwa katika sura na sauti ya chama cha siasa (CCM) na mtu binafsi (Rais wa Zanzibar) anayeonekana kama mhimili mkuu wa utoaji wa huduma za maendeleo.

Hata hivyo, tunaweza kusema kwamba dhana ya maendeleo, kama inavyoelezwa na bango hili na mabango mengine mengi wakati wa kampeni kali za uchaguzi ya 2025, kwa uhalisia, si sehemu ya mpango wa kisiasa au kiuchumi wa chama cha siasa: kuwapatia raia wa taifa huduma za kijamii za msingi (hasa elimu, huduma za afya, miundombinu ya usafiri, pamoja na usalama na haki) ndiyo sababu kuu ya kuwepo kwa serikali na hivyo basi ni mojawapo ya majukumu yake makuu, angalau katika muktadha wa kidemokrasia, bila kujali ni chama gani cha siasa au muungano upi ulio madarakani. Lakini katika nchi kama Tanzania, ambapo maisha ya kisiasa yamedhibitiwa tangu uhuru na ‘chama-dola’—yaani, na mfumo wa mamlaka uliojikita na ambao muundo ya serikali na chama cha CCM vimeunganishwa sana kiasi kwamba, licha ya kufanyika kwa mara kwa mara kwa uchaguzi wa vyama vingi tangu 1995, kwa hakika ni mfumo wa chama kimoja (Makulilo 2008; Paget 2019) pamoja na ubabe wa ushindani (competitive authoritarianism) (Levitsky & Way 2010; Morse 2014—kutokuwepo na mipaka wazi kati ya majukumu ya serikali na yale ya chama si jambo la kushangaza.

Kujenga miundombinu ama kuwawezesha wananchi?

Ongezeko la idadi ya watu haliwezi, peke yake, kueleza hitaji la shule mpya au hospitali mpya; kinacholielezea pia ni kushindwa kwa serikali—iwe serikali ya Muungano au serikali ya Zanzibar—kutimiza kikamilifu majukumu yake ya kiserikali na kuwezesha maono yake ya kidemokrasia kwa taifa. Tafiti za kitaaluma kuhusu maisha ya kisiasa na uchumi wa kisiasa wa Tanzania zimeonyesha, kwa miaka kadhaa sasa, kwamba mifumo iliyopo ya unyonyaji wa kiuchumi, ikijumuishwa na ongezeko la utawala wa ubabe wa kisiasa tangu mwaka 2015, imechangia kuwanufaisha matabaka ya kisiasa na kiuchumi yaliyopo kwa upande mmoja, huku ikiwaadhibu wananchi wa kawaida kwa upande mwingine, kwa kuwa huduma za msingi za jamii zimepuuzwa kwa kiasi kikubwa (Gray 2015). Ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya, inapofanyika, si mara zote huambatana na uteuzi au ajira kwa watu waliopata mafunzo ya kutosha na wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa viwango vya juu.

Katika miaka iliyofuata baada ya kupitishwa kwa ujamaa, rais wa kwanza wa Tanzania huru, Julius K. Nyerere, alisisitiza mara kwa mara kwamba hakuwezi kuwa na uhuru wa kweli—yaani, uhuru wa kitaifa, wa wananchi na wa mtu binafsi—bila maendeleo (Nyerere 1973, tazama pia Hunter 2015; Ahearne 2016). Lakini maendeleo hayakuhusu tu kujenga shule na hospitali, kusambaza umeme na maji, au kutumia matrekta na mbolea: vitu hivi vyote vinavyoonekana kwa macho kama nyenzo tu—nyenzo muhimu, lakini si za kutosha—za kile Nyerere alichokiita ‘maendeleo ya watu’, yaani maendeleo ya mwili na akili za wanawake na wanaume: kupata elimu ili kuelewa changamoto za dunia, lakini pia kufanikiwa katika taaluma aliyochagua, na kwa upana zaidi, maisha na malengo yake, pamoja na kuwa na afya njema na chakula cha kutosha, na lishe bora, ili asinyanyaswe sana na hali yake ya kimwili. Ingawa ‘mipango ya kujitegemea’ na ‘maendeleo shirikishi’ ilikuwa sehemu muhimu wa ajenda ya wakati huo, mtazamo wa juu-chini uliendelea kutawala katika nchi ambako taswira ya dola kama baba mlezi ilikuwa na nguvu; dola ikijitokeza kama mtoaji mkuu na wa mwisho wa huduma na ustawi wa wananchi (Green 2012; Mercer 2002). Tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, CCM imetumia msamiatio wa maendeleo kama mbinu endelevu ya kutafsiri kuwa madarakani kuwa uhalali wa kisiasa. Kwa mfano, mwaka 1995 maendeleo yaliwasilishwa kama mageuzi yaliyodhibitiwa—hasa mpito kuelekea uchumi wa soko. Katika Ilani ya CCM la 2010-2015, maendeleo yalielezewa kama kilimo, miundombinu, mipango, na utekelezaji unaopimika. Haya yalikuwa matendo ya kisera ya chama yaliyokusudiwa kuchochea maendeleo (Nguyahambi et al. 2019). Mwaka 2020, kauli ya CCM kuhusu maendeleo ilizidi kuwa ya kiutendaji na maonyesho tu: barabara, reli, miradi ya nishati, elimu ya bure, na miundombinu inayoonekana vilitumika kama ushahidi wa utawala.

Hasa Zanzibar—ambapo hadhi yake ya kujitawala kwa kiasi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (semi-autonomous) iliipa serikali na Baraza la Wawakilishi uhuru mkubwa kujiamulia katika sera za kiuchumi na kijamii— ahadi za maendeleo zimekuwa ahadi za ‘maendeleo ya kisasa’ dhidi ya historia ya kutengwa, dhuluma na mfumo ulio dhahiri wa matabaka ya rangi na hadhi. Kauli mbiu ya chama-dola kuhusu “matunda ya Mapinduzi”  imetumika kutambulisha mabadiliko hayo yanayoitwa ya ‘kisasa’. Chini ya Rais Abeid Amani Karume, maendeleo yalirejelea hasa uanzishwaji wa viwanda visiwani Zanzibar, ukuaji wa kilimo na ujenzi wa majengo ya kisasa ya makazi ya watu yaliyobuniwa na Wajerumani wa Mashariki, yaliyo na maji ya bomba, gesi na umeme—kwa mfano, eneo la makazi katika mtaa wa Michenzani (Myers 1994; De Nijs 2013). Maboresho hayo pia yalifika vijijini kupitia majenereta ya dizeli, pampu za maji, na televisheni (Winther 2008). Katika baadhi ya kumbukumbu za sasa, utawala wa kimapinduzi Zanzibar unawakilisha utulivu, utoaji mpana  wa huduma za kijamii, makazi, ajira, na mishahara mizuri (Bissell). Hata hivyo, kazi za kitaaluma zinaangazia hali duni ya kiuchumi ya miaka ya 1970 na 1980, wakati tabaka la juu lilijitajirisha (Roberts 2016). Siasa hii ya unyang’anyi ambapo “ukatili wa kisiasa ulikuwa sifa” (Othman 1995, 175) imeendelea hadi sasa (Cameron 2018). Na maendeleo kama usasa bado yanatawala fikra za tabaka la kisiasa na kiuchumi linaloongoza dola; sasa yakimaanisha majengo marefu yenye vioo vya rangi, makazi yaliyofungwa kwa usalama maalumu, maduka makubwa ya kisasa na barabara zenye madaraja ya juu (flyover). Katika Ilani ya CCM ya mwaka 2025, mgombea urais wa Zanzibar na Rais wa sasa Hussein Mwinyi alihitimisha ujumbe wake kwa wananchi wa Zanzibar kwa kusema:

Kwa heshima kubwa, naahidi kwamba, nitaongeza kasi ya maendeleo kwa kuimarisha vyanzo vya mapato, kukuza uchumi wa Zanzibar, na kuhakikisha wananchi wote wananufaika na huduma bora za jamii.

Kuwashawishi wapiga kura kupitia kampeni zenye msisitizo mkubwa wa mabango?

Mwaka 2005, kama katika chaguzi zilizopita, CCM ilitegemea kwa kiasi kikubwa mawasiliano ya picha kupitia mabango (visual communication) yaliyobandikwa kwenye kuta katika miji na vijiji vya Zanzibar, pamoja na mabango madogo na mabango makubwa ya matangazo. Nchi nzima ilipambwa kwa rangi ya kijani na njano, rangi za chama. Kampeni ya chama tawala, kilichokuwa kikitafuta kuchaguliwa tena, ilikuwa na ufadhili mkubwa. Mnamo Agosti 2025, miezi michache kabla ya uchaguzi, CCM ilikuwa imefanya kampeni ya kuchangisha fedha iliyokusanya zaidi ya shilingi bilioni 86 za Tanzania (takriban dola milioni 32 za Marekani) (Wambura, 2025), kwa michango mikubwa kutoka sekta binafsi na za uchimbaji madini—alama ya uhusiano wa karibu kati ya mitandao ya wasomi ndani ya mfumo wa chama-dola (Gray 2015; Morse 2019). Vipengele hivi vya mawasiliano ya picha (visual communication) vilifuatana na mikutano ya kisiasa ambapo aina zote za bidhaa za uchaguzi ziliuzwa au kusambazwa: khanga, fulana, kofia, mikoba na mifuko ya kubebea vitu, n.k. Bidhaa hizi za kisiasa zilizogeuzwa kuwa bidhaa za kibiashara ziliandaliwa kwa kuzingatia mapendeleo ya kijinsia, huku khanga, gauni au skafu zikiwa kwa wanawake na fulana na kofia kwa wanaume. Pia ililenga wapiga kura wenye uwezo mdogo wa kifedha: kulikuwa na aina mbalimbali za bidhaa zilizouzwa kwa bei nafuu, kama vile pini au beji. Katika nchi ambapo mikutano ya kampeni ni jambo la kawaida (Paget 2019, 2024), ni muhimu kuyatazama mawasiliano ya picha (visual communication), vifaa vya uchaguzi na mikutano ya kampeni kwa pamoja kama maonyesho ya nguvu ya kisiasa, ambayo kupitia kwake chama-dola hujaribu kuwashawishi wapiga kura.

Kama nyenzo ya uhamasishaji wa kisiasa, mabango ya uchaguzi, kama yalivyo mabango ya matangazo ya kibiashara, yanapata manufaa yao katika “uwezo wao mkubwa wa kushawishi” (Sontag 1970) kwa kutegemea zaidi picha kuliko maandishi pamoja kwa kudumu kwao kwa muda mrefu, kwa kuwa hubandikwa kwa wiki kadhaa, na wakati mwingine kwa miezi. Maeneo la mijini ya Zanzibar yamegeuka kuwa ishara ya alama za uchaguzi, hasa mabango ya uchaguzi, kwani mabango mapya yanabandikwa juu ya yale ya zamani, kiasi kwamba mabango kadhaa kutoka kwa chaguzi tofauti huweza kuwepo kwa pamoja. Mabango haya pia hupata ufanisi wake kutokana na hulka yake ya kuonekana dhahiri: haiwezekani kutoyaona. Vipengele vya kuvutia vya picha vinakusudia kuvutia macho ya watu lakini pia kushinda mvuto wa ushindani kutoka kwa mabango ya vyama vya upinzani. Hata hivyo, mtu anaweza kujiuliza iwapo, katika nafasi iliyojaa mabango kiasi hiki, picha na kauli mbiu za uchaguzi bado zinafanikiwa kufikia malengo yake la kuwashawishi wapiga kura. Kama ilivyo kwa minara za ukumbusho (monuments), mabango hayo yanakabiliwa na kitendawili fulani: hayawezi kupuuzwa kabisa, lakini yanaweza kusahaulika kwa urahisi au kukutana na hali ya watu kutojali. Kwa kumnukuu kwa ufupi Robert Musil, akizungumzia minara ya ukumbusho (monuments), “hakuna kitu duniani kisichoonekana kama (mabango ya uchaguzi). (…) yamejaa kitu fulani kinachofukuza umakini, na kufanya macho yapite juu yake bila kuyashika, kama matone ya maji yanavyotiririka kwenye turubai, bila hata kusita kwa muda mfupi” (Musil 2006 [1936], tazama pia Fouéré 2017). Ingawa ikiwa ni bango la kipekee na likiwa moja sehemu fulani basi linaweza kuwa na athari kubwa katika mazingira maalum (Fouéré 2016), katika hali nyingi, mabango yaliyosanifishwa kwa mtindo mmoja ni mkakati mwingine tu wa kuhamasisha na kuwashawishi wapiga kura jambo ambalo wapiga kura wengi huwa hawatilii maanani.

Kuona, kuzungumza na kufikiria maendeleo miongoni mwa wapiga kura

Je, lugha ya CCM kuhusu maendeleo imesikikaje, imetwaliwaje, imeingizwa vipi katika fikra za wananchi, au, kinyume chake, imepingwa vipi—kimyakimya au kwa sauti zaidi—katika mazungumzo ya kila siku ya kisiasa mwaka 2025?[5] Kwa wengi wa wahojiwa wetu katika siku za mwisho za kampeni na siku ya uchaguzi, uhusiano kati ya chama tawala CCM na maendeleo ulionekana si tu kuwa na mantiki, bali pia kuwa jambo lililojidhihirisha lenyewe. Mwanamke mwenye umri wa miaka 28 kutoka Unguja, akitafakari mabadiliko ya hivi karibuni katika eneo lake, alieleza:

Kwangu mimi, Chama Cha Mapinduzi (CCM) huleta maendeleo nchini: katika miaka ya hivi karibuni, barabara, shule, na hospitali zimejengwa, na kutolazimika kulipia huduma za afya ni uboreshaji mkubwa.

Kwa mtazamo wa juu juu, mtazamo wa mwanamke huyu unaonekana kuthibitisha mafanikio ya ya kiutawala kwa CCM. Anabainisha vipengele vinavyoonekana ambavyo wagombea kisiasa wamekuwa wakivitumia kwa maneno, na ambavyo wapiga kura, kama mwanamke huyu wa miaka 28, huviangalia haraka. Ni wazi kwamba sarufi ya mabango inaakisiwa katika maisha ya kila siku ya kijamii ya watu. 

Ile hali ya kumangazia sana mtu (personalization) kwenye mabango pamoja na kutafuta maana huonekana kupitia mwanamke wa miaka 53 aliyeeleza yafuatayo: 

Nataka Hussein Ali Mwinyi aendelee kuwa kiongozi wetu kwa sababu analeta maendeleo. Ametimiza mambo mengi makuu, ikiwemo kujenga masoko na hospitali na kuboresha nyanja nyingi za jamii yetu.

Hapa, maendeleo si ya vitu tu—yamejidhihirisha na kuonekana kupitia mfano na taswira ya rais na chama. Hussein Ali Mwinyi anakuwa mpatanishi ambaye kupitia kwake utoaji wa huduma za serikali unaonekana na kufasiriwa.

Kwa wengine, historia zilizojengeka za visiwa hivi, pamoja na mahusiano ya kifamilia, hufanya uhusiano na maelezo kuhusu maendeleo unatolewa na CCM kutokuwa na umuhimu. Iwe kuna maendeleo au hakuna, kura yao itabaki kuwa ya CCM. Hii inaonekana katika mazungumzo na mwanamke mwenye umri wa miaka 45 aliyesema: 

Mimi ni mama anayekaa nyumbani. Nimekipenda Chama Cha Mapinduzi tangu niweze kukumbuka, na siasa daima zimekuwepo katika familia yangu. Nimekuwa nikipiga kura tangu mwishoni mwa miaka ya 1990. Namheshimu rais wa sasa (Hussein Ali Mwinyi) kwa sababu ya miundombinu mipya aliyoiweka: shule, masoko, na huduma zingine. Nataka miaka mitano zaidi na rais huyu.

Ni wazi kwamba, kwa baadhi ya wafuasi wa CCM, kama si wote, upigaji kura hauhusu tu ahadi ya maendeleo, bali ni chaguo linalotokana na urithi, uaminifu wa kisiasa, na mapenzi ya kihisia. Maendeleo, kwa maana hii, hufanya kazi kama daraja kati ya yaliyopita na yaliyopo sasa—yakiunganisha mshikamano wa vizazi na ujumbe wa kisiasa wa kisasa.

Ushahidi zaidi wa hili unaweza kuonekana kutoka kwa Mbunge wa CCM wa Jimbo la Mpendae, Toufiq Salim Turky ambaye alikuwa mbunge kufuatia kifo cha baba yake, Salim Turky, wiki chache kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020. Wakati huo, Salim Turky alikuwa mgombea wa CCM. Toufiq Turky alituambia, kujenga miundombinu na kufanya huduma za umma zipatikane kwa kila mtu kunamaanisha kwamba CCM inawahudumia watu wote, na siyo wenye uwezo pekee, akibainisha kwamba: 

Leo, jimbo letu la uchaguzi liko miongoni mwa bora zaidi kwa upande wa miundombinu. Upatikanaji wa maji, utendaji wa shule… (…) Sera za CCM ni za kujumuisha wote. Hospitali za bure, barabara mpya, na elimu zinapatikana kwa kila mtu, siyo kwa matajiri pekee.

Dondoo hizi, licha ya ufupi wake, zinaonesha kwamba maendeleo yanaeleza jambo kubwa zaidi kuliko ujenzi wa miundombinu. Ni kiashiria kinachobadilika na chenye maana nyingi, kinachowezesha kuzungumzia uaminifu wa kifamilia, mshikamano wa kihisia, ubinafsishaji wa mamlaka, taabu za kawaida za maisha, na matarajio ya maisha bora. Kwa namna nyingine, ikiwa maendeleo yanafanya kazi kama teknolojia ya kisiasa ambayo kupitia kwayo CCM hutafuta uhalali wa kisiasa—au hata ubabe wa kisiasa pale upigaji kura unapogeuzwa kuwa tendo la utii—ni kwa sababu maendeleo yamefungamana na baadhi ya nguzo muhimu za maisha ya kijamii visiwani Zanzibar: yakiwemo yale ya kifamilia na mahusiano ya kijamii, heshima na utu, urithi na urithishaji wa kumbukumbu za kisiasa. Hata hivyo, kama wanavyotukumbusha Nguyahambi et al. (2019, uk. 85), “Dhana ya maendeleo pia hutumika kuziondolea uhalali sauti za ukosoaji, kwa kuwa mtu yeyote asiyeunga mkono njia ya sasa iliyoainishwa na wenye mamlaka anaweza kuwasilishwa kama mpinga maendeleo na mpinga ustawi wa wananchi wa nchi kwa ujumla.” Kwa maneno mengine, kwa mtazamo wa CCM, wale wasiokumbatia maono yake ya maendeleo huwekwa katika nafasi ya maadui wa taifa.

Mfululizo huu wa makala ya Mambo! unajikita katika kuelezea mwaka wa uchaguzi wa 2025 nchini Tanzania. Unatoa maelezo ya kipekee wa usomaji wa kina na ukaribu wa vielelezo vya matukio ya kisiasa ya mwaka huu wa uchaguzi, uliokua na matukio mengi na uliotawaliwa na muendelezo wa ukandamizaji wa serikali. Katika kila sehemu cha mfululizo huu, tukio lililochaguliwa linazalishwa tena katika asili yake na kutafsiriwa panapohitajika, likiwekwa katika muktadha kwa uangalifu na kufafanuliwa au kupewa maelezo ya karibu kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa kuelewa kwa kina sehemu lilipotokea pamoja na maana na umuhimu wake. Matukio haya ni vyanzo ama nyaraka ya maana kwa ajili ya kuchambua muendelezo wa utawala wa kimabavu na ukandamizaji wa wazi uliofanywa na serikali ya Tanzania katika kipindi hiki cha uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2025.

Marejeo

Ahearne, R.M. (2016). Development and progress as historical phenomena in Tanzania: “Maendeleo? We had that in the past.” African Studies Review 59(1), 77-96. https://www.jstor.org/stable/24805943

Bissell, W. C. (2005). Engaging Colonial Nostalgia. Cultural Anthropology 20(2), 215-248. https://doi.org/10.1525/can.2005.20.2.215

Cameron, G. (2018). Zanzibar in the Tanzania Union. In L. de Vries, P. Englebert, & M. Schomerus. Secessionism in African Politics (p. 178-205). Palgrave Macmillan. https://doi.org/10.1007/978-3-319-90206-7_7

De Nijs, A. (2013). Lessons from “The Other side”. Post-colonial ideals and everyday inhabitation in the Michenzani blocks, Zanzibar. Planum. The Journal of Urbanism 26(1). http://media.planum.bedita.net/ff/89/03_CTBT2012_by_Planum_no_26-2013_De-Nijs_Section_1-1.pdf

Fouéré, M.-A. (2016). The election poster: Art, strategy, and matter for politics. The revolution, the opposition, and the 2015 elections in Zanzibar. Politique africaine 144(4), i-xix. https://doi.org/10.3917/polaf.144.0115

Fouéré, M.-A. (2017). Malaise monumental, inconfort commémoratif. Zanzibar et sa Tour de la Révolution [Monumental Uneasiness, Commemorative Discomfort. Zanzibar and its Revolution Tower]. Cahiers d’Études africaines 227(3), 583-618. https://doi.org/10.4000/etudesafricaines.20830

Gray, H. S. (2015). The political economy of grand corruption in Tanzania. African Affairs, 114(456), 382–403.

Green, M. (2012). Anticipatory development: Mobilizing civil society in Tanzania. Critique of Anthropology 32(3), 309-333. 10.1177/0308275X12449107

Hunter, E. (2015). Political thought and the public sphere in Tanzania: Freedom, democracy and citizenship in the era of decolonization. Cambridge University Press.

Koponen, J. (2018). Maendeleo: From colonial to postcolonial development in Tanzania. Tanzania Zamani 10(1), 1.

Laclau, E. & Mouffe, C. (1985). Hegemony and Socialist Strategy. Towards a Radical Democratic Politics. Verso (1st ed.).

Levitksy, S., & Way, L. (2010). Competitive authoritarianism: Hybrid regimes after the Cold War. Cambridge University Press.

Makulilo, A. (2008). Tanzania: A de facto one party state? VDM Verlag.

Mercer, C. (2002). The discourse of maendeleo and the politics of women’s participation in Mount Kilimanjaro. Development and Change 33(1), 101–127. https://doi.org/10.1111/1467-7660.00242

Morse, Y. L. (2014). Party matters: The institutional origins of competitive hegemony in Tanzania. Democratization, 21(4), 655-677. https://doi.org/10.1080/13510347.2013.764285

Musil, R. (2006 [1936]). Posthumous Papers of a Living Author. Archipelago Books.

Myers, G. A. (1994). Making the Socialist City of Zanzibar. Geographical Review 84(4), 451-464. https://www.jstor.org/stable/215759

Nguyahambi A.M., Chang’a H.H., Matunga B.N., Kilonzo R.G., Kontinen T. (2019). In K. Holma & T. Kontinen, Contextualizing citizenship in Tanzania. Practices of citizenship in East Africa (p. 73-89). Routledge. https://scispace.com/pdf/contextualizing-citizenship-in-tanzania-527a2wzp8r.pdf

Nyerere, J. K. (1973). Freedom and development/Uhuru na maendeleo, A Selection from writings and speeches 1968-1973. Oxford University Press. https://www.juliusnyerere.org/uploads/uhuru_na_maendeleo.pdf

Othman, H. (1995). The Union with Zanzibar. In C. Legum & G. Mmari, Mwalimu. The Influence of Nyerere (p. 170-175). James Currey, Mkuki na Nyota, Africa World Press.

Paget, D. (2024). Capitalized rallies: why campaigns costs are rising and rallies are hybridizing in Tanzania. Party Politics 30(5), 908-919. https://doi.org/10.1177/13540688231190033

Paget, D. (2019). The Rally-Intensive Campaign: A Distinct Form of Electioneering in Sub-Saharan Africa and Beyond. The International Journal of Press/Politics 24(4), 444-464. 10.1177/1940161219847952.  

Roberts, G. (2016). Politics, decolonisation, and the Cold War in Dar es Salaam c. 1965-72. PhD Diss., University of Warwick, Department of History.

Sontag, S. (1970). Posters: Advertisement, Art, Political Artifact, Commodity. In D. Stermer, The Art of Revolution: 96 Posters from Cuba. McGraw-Hill.

Wambura, B. (2025, August 13). Tanzanian tycoons, miners and leaders give CCM over Sh86 billion for 2025 campaign, party building. The Citizen. https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/news/tanzanian-tycoons-miners-and-leaders-give-ccm-over-sh86-billion-for-2025-campaign-party-building-5153100

Winther, T. (2008). The Impact of Electricity: Development, Desires and Dilemmas. Berghahn Books.


Maelezo

[1] Tunafuata mtazamo wa Ernesto Laclau na Chantal Mouffe (2001), ambao unaangazia kwamba dhana—au alama—hazina maana maalum iliyoshikiliwa nazo, bali maana zisizo wazi, zinazobadilika, na zenye kutofautiana, ambazo zimejaa maana zilizojengwa kihistoria na zinaweza kutofautiana na kuumbwa upya kulingana na matukio na muktadha wa matumizi yake. Hata hivyo, watu—na katika kesi yetu, taasisi na mashirika, kama vile serikali au vyama vya siasa—hufanya juhudi za kuendelea kuunda maana thabiti, au “vituo vya kiungo” (Ibid: 112).

[2] Kupitia wasilisho letu kwa lugha ya Kiingereza, tunatumia kwa makusudi neno la Kiswahili maendeleo kwa kuwa ni dhana ya ndani (emic) ambayo tafsiri yake kama ‘maendeleo’ (wakati mwingine ‘maendeleo ya kisasa’), ingawa ni muhimu na inafaa, inashindwa kuakisi kikamilifu maana zake tata, zinazobadilika, na zinazotegemea historia

[3] Uchambuzi uliowasilishwa hapa unategemea utafiti wa nyanjani uliofanywa Zanzibar na Ania Gruca, Nicodemus Minde na Marie-Aude Fouéré wakati wa kipindi cha uchaguzi cha 2025, ukichanganya uchunguzi wa karibu wa vifaa vya kampeni na mahojiano mafupi yaliyofanywa maeneo mbalimbali katika visiwa vya Unguja na Pemba katika wiki zilizotangulia Siku ya kupiga kura wa 29 Oktoba. Mahojiano haya mafupi yalifanywa na wapiga kura wa rika, taaluma, na mwelekeo tofauti wa kisiasa.

[4] Tazama pia Sehemu ya 3 “Miili ya kigeni, vijana waliopotoshwa: Hotuba ya kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan, 3 Novemba 2025” (https://mambo.hypotheses.org/5457).

[5] Kwa ushuhuda zaidi kuhusu matarajio ya kisiasa na chaguzi za uchaguzi, ikiwemo kutoka kwa wafuasi wa upinzani, tazama ripoti ya picha ya Ania Gruca inayohusiana na kipindi hiki, “Kutoka matumaini hadi shaka. Sauti za Wazanzibari.”

Marie-Aude Fouéré
Marie-Aude Fouéré
Nicodemus Minde
Nicodemus Minde
Nico Minde is doctoral student in International Relations at the United States International University – Africa (USIU – Africa) Nairobi,… Lire la suite

OpenEdition vous propose de citer ce billet de la manière suivante :
Marie-Aude Fouéré, Nicodemus Minde (7 mai 2026). Sehemu ya #5. ‘Kura ni alama ya maendeleo’: Kuahidi maendeleo Zanzibar kupitia kampeni zilizotawaliwa na mabango ya kisiasa. Mambo ! Consulté le 12 juin 2026 à l’adresse https://doi.org/10.58079/166xj


Vous aimerez aussi...

Laisser un commentaire

Votre adresse e-mail ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.